• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Mwanamume na wanafunzi wawili waangamia kisimani

Mwanamume na wanafunzi wawili waangamia kisimani

Na OSCAR KAKAI

MWANAMUME mwenye umri wa kadri na wanafunzi wawili wa shule ya msingi mnamo Ijumaa walifariki baada ya kuanguka katika kisima katika Shule ya Msingi ya Chewoyet, Kaunti ya Pokot Magharibi.

Wanafunzi hao wawili wa darasa la nane walikuwa wakiteka maji na walijaribu kuondoa ndoo waliyokuwa wakitumia kabla ya kutumbukia ndani na kufa.

Mmoja wa wanafunzi aliingia kwenye kisima hicho cha futi 40 lakini akashindwa kuondoka ndipo mwenzake akamfuata na wawili hao kufa maji kisimani humo.

Juhudi za mwanamume fundi wa mbao kuwaondoa kisimani pia ziliishia katika kifo kwa kuwa kamba aliyokuwa akitumia kuingia kisimani ilikatika naye pia akafa majini.

Juhudi za maafisa wa uokoaji wa kaunti, polisi na maafisa wa Msalaba Mwekundu kuondoa miili hiyo majini zilikosa kuzaa matunda na ikambidi mkazi Leonard Kasighyo Kamosin kuokoa hali kwa kuingia kisimani na kuwatoa watatu hao.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi Jackson Tumwet alisema wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho.

“Mwanaume huyo alitaka kuwaokoa watoto hao lakini pia akafa. Ni jambo la kusikitisha sana,” akasema Bw Tumwet.

Mkazi Lucy Lotee alitoa wito kwa serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa visima vyote kwenye shule ni salama kwa wanafunzi wanapochota maji na wasitumie ndoo kuyateka maji.

You can share this post!

Kuzimwa kwa BBI kulivyovuruga siasa za urithi 2022

Walionufaika na kupoteza kwa uamuzi wa korti kuhusu BBI