• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mwili wa aliyetekwa nyara Naivasha wapatikana Thika familia ikitaka uchunguzi wa kina

Mwili wa aliyetekwa nyara Naivasha wapatikana Thika familia ikitaka uchunguzi wa kina

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI inastahili kuingilia kati ili kujua kiini cha mauaji ya kiholela yanayozidi kushuhudiwa nchini, amesema naibu mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa, Bi Salma Hemed, akilaani tukio la kupotea kwa John Maina mkazi wa Naivasha katika hali ya kutatanisha.

Ilidaiwa kuwa mnamo Novemba 31, 2021, John Maina na rafiki yake walikodisha gari dogo ili watumie kuenda kuhudhuria kesi fulani katika mahakama ya Naivasha.

Kulingana na familia yake marehemu, alipotoweka walilazimika kuzuru vituo kadha vya polisi kutafuta mwili wake bila mafanikio yoyote.

Kulingana na Bi Hemed ni kwamba maafisa wa Haki Africa pamoja na familia walifuatilia kesi hiyo na kugundua ya kwamba mwili wa marehemu ulikuwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha General Kago, katika hospitali  ya Thika Level 5 mjini Thika.

“Polisi wanastahili kuwa mstari wa mbele kuwasadia wananchi wakati wa shida. Familia ya marehemu ilimtafuta katika vituo kadha vya polisi na hatimaye mwili ukapatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti mjini Thika,” alilalamika mkurugenzi huyo.

Kulingana na ripoti ya daktari mkuu wa upasuaji Dkt Johansen Oduor, mkono wa kushoto wa mhanga ulikuwa umekatwa na vile vile mguu wake, huku sehemu zake za siri zikiwa zimenyofolewa.

Aidha, Bi Hemed alitaka serikali kuwa macho hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

“Kuna haja ya serikali kuweka usalama wa kutosha na kuwa macho ili kuwalinda wananchi kutokana na utekaji nyara,” alifafanua naibu mkurugenzi huyo.

Babake marehemu, Bw Samuel Kariuki, alisema mwanawe alipotea kutoka Novemba 31, 2021, na maiti yake kupatikana Desemba 26, 2021 katika chumba cha kuhifadhi maiti cha General Kago, mjini Thika.

Bw Kariuki alieleza kuwa marehemu wakati wa mwisho wa uhai wake alikuwa amehudhuria kesi fulani katika mahakama ya Naivasha, lakini baadaye yeye na mwenzake walitekwa nyara.

Kulingana na ripoti ya polisi marehemu na rafikiye mwanaume walitekwa nyara na wakafanyiwa unyama kisha miili yao ikatupwa katika mto Tana eneo la Masinga, kaunti ya Machakos.

Hata hivyo gari walilokuwa nalo lilipatikana Gilgil, likiwa limeegeshwa kando ya barabara.

Bakake Maina ambaye ni marehemu anaiomba serikali kuingilia kati ili kuwanasa washukiwa waliotenda kitendo hicho kibaya.

Naye Bw Dickson Kariuki ambaye ni nduguye marehemu anataka serikali kuingilia kati na kujua ukweli wa mambo.

“Tunashangaa kuona ndugu yetu ameuawa kutoka Naivasha na mwili wake kupatikana katika mochari ya Thika,” alieleza nduguye marehemu.

Aliiomba serikali kufanya hima kuona ya kwamba haki inatendeka ili kujua ukweli wa mambo.

“Kulingana na jinsi mwili huo ulivyo, inaonyesha wazi ndugu yetu alitekwa nyara na kuuawa kinyama kwa sababu kichwa chake kilipondwa na kifaa butu kwa nyuma jambo lililofanya avuje damu kwa wingi,” alifafanua Bw Kariuki.

Kile ambacho familia hiyo inaomba ni haki itendeke kwa sababu inaonekana kuna kikundi cha watu fulani ambao wameamua kuangamiza wananchi kiholela.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti 22 zilivyotafuna hela za wananchi

Michirizi mwilini na namna ya kuiondoa

T L