• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Nassir ndani naye Sonko akikazana

Nassir ndani naye Sonko akikazana

WINNIE ATIENO NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, amesisitiza atawasilisha hati zake kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufanyiwa utathmini wa kuwania ugavana Mombasa.

Tume hiyo inayotarajiwa kufunga shughuli za kutathmini wagombeaji ugavana Mombasa leo, ilikuwa imemratibisha Bw Sonko kuwasilisha hati zake za uwaniaji leo kabla mwenyekiti, Bw Wafula Chebukati, kutangaza uamuzi wa kumzima kwa sababu za kimaadili.

“Tutakuwa Mombasa kesho. Wasiomtaka Sonko Mombasa itabidi wameze wembe. Mungu akipenda tutakuwa hadi debeni Agosti 9,” wakili wake, Bw Jared Magolo, alisema Jumatatu.

Kulingana na mawakili wake, endapo afisa mkuu wa IEBC atakataa karatasi hizo, wataenda kwa jopo la kutatua mizozo inavyohitajika kwa sheria za uchaguzi na jopo likimkataa atarudi mahakamani.

Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, ambaye ni mgombea mwenza wake, aliashiria atatafuta kibali cha kisheria kuchukua mahali pa Bw Sonko ikiwa IEBC itashikilia msimamo wake.

Jana, Jaji Jairus Ngaah wa Mahakama Kuu mjini Nairobi, aliagiza kesi ambapo Bw Sonko ameshtaki IEBC kwa kumzima kuwania, ipelekwe kwa Mahakama ya Mombasa.

Bw Mbogo ambaye awali aliazimia kuwania kiti hicho, alishawishiwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko baadaye kupitia Chama cha Wiper.

“Itabidi nitafute mgombea mwenza, lakini bado tuna muda wa kutosha kutekeleza jambo hilo mara moja,” alisema.

Kesi nyingi zimewasilishwa katika mahakama tofauti nchini kuhusu iwapo Bw Sonko anastahili kuwania kiti cha kisiasa baada ya kutimuliwa Nairobi.

Jopo la majaji watatu liliteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome kuamua kesi nane kati ya hizo. Jopo hilo linaongozwa na Jaji David Majanja huku majaji wengine wakiwa ni Chacha Mwita na Mugure Thande.

Akiwakilishwa na mawakili Assa Nyakundi, John Khaminwa, Jared Magolo, na Tutis Kirui, Bw Sonko alipinga mahakamani hatua ya IEBC kumkataza kuwania ugavana Mombasa.

Kwingineko, Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, anayewania ugavana Mombasa kupitia kwa ODM, jana alikuwa wa kwanza kuidhinishwa na IEBC.

Wagombeaji wengine ambao walikuwa wamepangiwa kutathminiwa tangu wikendi walipatikana kuwa na kasoro katika stakabadhi zao, wakapewa muda kuzirekebisha.

Kwa upande mwingine, aliyekuwa seneta, Bw Hassan Omar, alisemekana alikuwa ameomba muda zaidi na anatarajiwa kufika mbele ya IEBC leo.

Bw Nassir ambaye aliandamana na mgombea mwenza wake, Bw Francis Thoya, alisema kuidhinishwa kwake ni mwanzo wa safari ya kuletea wakazi wa Mombasa mabadiliko katika maisha yao.

“Tutahakikisha huduma za serikali zinawafikia watu mashinani ili kila mtu anufaike na ugatuzi vijijini. Safari ndio imeanza ya kuhakikisha matarajio ya wakazi wa Mombasa yanatimizwa kupitia manifesto yetu,” alisema Bw Nassir.

Baadaye aliungana na wanasiasa wa Mombasa akiwemo wabunge, Badi Twalib (Jomvu), Mohammed Faki (seneta), viongozi wa ODM na wafuasi wake katika ukumbi wa Lohana kusherehekea hatua aliyopiga katika azma yake.

  • Tags

You can share this post!

Pigo Pwani Oil ikilazimika kusitisha shughuli zake

Ronaldo asaidia Ureno kuzamisha Uswisi katika pambano la...

T L