• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Natembeya aagiza vituo vya pombe vifungwe kijijini Hodi Hodi

Natembeya aagiza vituo vya pombe vifungwe kijijini Hodi Hodi

Na SAMMY WAWERU

MRATIBU wa eneo la Bonde la Ufa George Natembeya ameamuru kwamba vituo vyote vya pombe vifungwe kijijini Hodi Hodi, Nakuru kufuatia kufariki kwa watu 10 waliokunywa pombe yenye sumu.

Vituo vilivyoathirika na amri hiyo ni vile vya kuuza pombe ya viroba au mifuko ya plastiki na ile ya chupa na hata kumiminiwa ili wateja wabebe hadi nyumbani.

Bw Natembeya alitoa amri hiyo Alhamisi, katika ziara yake kijiji cha Hodi Hodi ambapo aliongoza operesheni kuvamia maeneo yaliyodaiwa kutengeneza na kuuza pombe haramu.

“Maafisa wa polisi na viongozi wengineo husika wa serikali wawajibike katika utendakazi,” akasema afisa huyo.

Idara ya polisi eneo hilo inanyooshewa kidole cha lawama, kwa kuzembea kazini na kuchangia kurejea kwa pombe haramu.

Bw Natembeya alieleza wasiwasi wake, akisema huenda wanakijiji wanatishiwa na watengenezaji pombe haramu hivyo wanaogopa kuwafichua.

“Inaonekana watu wameanza kutishwa na wahusika wa pombe haramu. Tangu tuje hapa watu wamesalia kimya,” akasema.

Baadhi ya majengo ya wauzaji pombe haramu yalibomolewa, kufuatia ziara ya Bw Natembeya.

Watu 16 walionusurika na unywaji wa pombe haramu wanaendelea kupata matibabu.

Waathiriwa wanasemekana kubugia mvinyo huo mnamo Jumatatu, na kufikia jioni baadhi yao kuanza kutapika, wakilalamikia maumivu ya tumbo.

“Miongoni mwa waliofariki ni mgema. Baadhi walipatana sehemu tofauti wakiwa wamepoteza fahamu,” akasema Bw Joseph Kuria, mmoja wa viongozi wa mpango wa Nyumba Kumi eneo hilo.

Mwanamke mjamzito pia ni kati ya waliofariki, baada ya kunywa kileo hicho hatari.

Kulingana na idara ya afya Nakuru, 16 ya walionusurika wamelazwa hospitalini, wakiendelea kupokea matibabu.

Huku uchunguzi ukianzishwa, idara ya polisi na chifu eneo hilo wamelaumiwa kwa kuzembea kukabili kurejea kwa pombe haramu.

Tukio la Nakuru, limejiri siku chache baada ya gazeti la Daily Nation kufichua kurejea kwa pombe haramu maeneo mbalimbali eneo la Bonde la Ufa.

Kaunti za Nakuru, Narok, Nyandarua, Kericho, Laikipia na Baringo kati ya nyinginezo zilitajwa kurejea kwa pombe haramu na ambayo ni hatari, kusababisha maafa na kufanya vijana kuwa mateka wa mvinyo na pombe.

You can share this post!

Mtaalamu awaponda akina mama wanaodai wana maziwa kidogo

Rekodi nyingine katika soka ya Uingereza baada ya Chelsea...