• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Rekodi nyingine katika soka ya Uingereza baada ya Chelsea kumsajili Lukaku kwa Sh15.2 bilioni

Rekodi nyingine katika soka ya Uingereza baada ya Chelsea kumsajili Lukaku kwa Sh15.2 bilioni

Na MASHIRIKA

CHELSEA wamemsajili upya fowadi Romelu Lukaku, 28, kutoka Inter Milan ya Italia kwa Sh15.2 bilioni.

Nyota huyo raia wa Ubelgiji anarejea uwanjani Stamford Bridge kwa mkataba wa miaka mitano baada ya kuondoka Chelsea na kujiunga na Everton kwa Sh4.3 bilioni mnamo 2014.

Kiasi hicho cha fedha kinakaribiana sana na Sh15.6 bilioni ambazo Manchester City waliweka mezani kwa kiungo raia wa Uingereza, Jack Grealish kutoka Aston Villa.

“Nilikuja hapa nikiwa mtoto wa umri mdogo sana. Sasa narejea kambini mwa kikosi hicho nikijivunia tajriba pana na ukomavu zaidi,” akasema Lukaku.

“Nimekuwa shabiki wa Chelsea tangu utotoni na hakuna chochote kinachonipa furaha kuliko kurejea katika klabu hii na kuisaidia kutwaa mataji zaidi,” akaongeza.

Fedha nyingi zaidi kwa sasa zimetumika kwa ajili ya Lukaku kuliko mchezaji yeyote mwingine katika historia huku klabu zote ambazo zimewahi kujivunia huduma zake zikiweka mezani jumla ya Sh45.2 bilioni katika nyakati mbalimbali.

Ilivyo, ina maana kwamba mbili kati ya ada za juu zaidi kuwahi kutolewa ili kusajili mchezaji katika soka ya Uingereza zimekuwa kwa ajili ya Lukaku.

Lukaku ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Ubelgiji (mabao 64), ndiye mwanasoka wa tatu ghali zaidi kuwahi kusajiliwa katika historia ya soka ya Italia alipojiunga na Inter Milan kutoka Manchester United kwa Sh11.5 bilioni mnamo 2019. Sasa ndiye mchezaji ghali zaidi kuwahi kuuzwa na klabu ya Serie A.

Chelsea ambao walitawazwa wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2020-21, walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya nne baada ya kufunga mabao 58. Mabao hayo yaliwaweka katika nafasi ya nane kwenye orodha ya vikosi vilivyopachika wavuni idadi kubwa zaidi ya magoli.

Mjerumani Timo Werner aliyesajiliwa kwa Sh7.5 bilioni mnamo Juni 2020 alichangia mabao sita pekee kutokana na jumla ya mechi 35 za EPL.

Kutua kwa Lukaku kambini mwa Chelsea kunatarajiwa kuchochea zaidi kuhama kwa fowadi Tammy Abraham, 23, anayewaniwa pakubwa na AS Roma pamoja na Arsenal. Chelsea wanatarajiwa pia kuagana rasmi na mshambuliaji Michy Batshuayi anayehemewa na vikosi kadhaa nchini Uturuki.

Lukaku alipoingia Chelsea kwa mara ya kwanza, alilinganishwa na nguli Didier Drogba ambaye alicheza pamoja naye kwa muda mfupi ugani Stamford Bridge.

Hata hivyo, alifungia kikosi hicho bao moja pekee kutokana na mechi 15 katika kipindi cha misimu mitatu.

Japo Lukaku alifichua mwishoni mwa msimu uliopita kwamba anafurahia maisha yake ugani San Siro, nyota huyo raia wa Ubelgiji aliwataka Inter mwanzoni mwa wiki hii kumuachilia ajiunge upya na Chelsea.

Lukaku aliwahi kuchezea Chelsea kati ya 2011 na 2014 japo miwili kati ya misimu hiyo ilimshuhudia akichezea West Bromwich Albion na Everton kwa mkopo.

Marejeo ya Lukaku ugani Stamford Bridge muhula huu yanafanyika miaka saba tangu aagane na Chelsea na kuyoyomea Everton waliompokeza mkataba wa kudumu mnamo 2014.

Nusura Lukaku ajiunge upya na Chelsea mnamo 2017 ila akahiari kuingia katika sajili rasmi ya Manchester United kwa Sh11.7 bilioni.

Lukaku alifunga mabao 47 katika jumla ya mechi 72 za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) katika kipindi cha zaidi ya misimu miwili ugani San Siro na akasaidia Inter kuzoa taji la kwanza la Serie tangu 2009-10 muhula uliopita.

Lukaku alijiunga na Chelsea kwa mara ya kwanza kutoka Anderlecht akiwa na umri wa miaka 18 kabla ya maarifa yake kutwaliwa na Everton kwa Sh4.3 bilioni.

Alifungia Everton mabao 53 kutokana na mechi 110 za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kabla ya Man-United kumfanya sogora wa pili ghali zaidi katika historia ya soka ya Uingereza walipomsajili mnamo Julai 2017.

Miaka miwili baada ya kufungia Man-United mabao 42 kutokana na mechi 96, Lukaku alijiunga na Inter kwa rekodi ya Sh11.5 bilioni.

Chelsea walikuwa wakihusishwa pakubwa na fowadi Erling Braut Haaland wa Borussia Dortmund mwishoni mwa msimu wa 2020-21. Hata hivyo, walianza kumhemea Lukaku baada ya kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kushikilia kwamba hakikuwa na azma ya kumtia mnadani sogora huyo raia wa Norway mwenye umri wa miaka 21.

WANASOKA GHALI ZAIDI KATIKA SOKA YA UINGEREZA:

Jack Grealish (Aston Villa hadi Manchester City) – Sh15.6 bilioni.

Romelu Lukaku (Inter Milan hadi Chelsea) – Sh15.2 bilioni.

Paul Pogba (Juventus hadi Manchester United) Sh13.8 bilioni.

Harry Maguire (Leicester City hadi Manchester United) – Sh12.4 bilioni.

Romelu Lukaku (Everton hadi Manchester United) – Sh11.7 bilioni.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Natembeya aagiza vituo vya pombe vifungwe kijijini Hodi Hodi

Cherargei akashifu Uhuru baada ya wanariadha waliowasili...