• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 10:30 AM
Mtaalamu awaponda akina mama wanaodai wana maziwa kidogo

Mtaalamu awaponda akina mama wanaodai wana maziwa kidogo

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA umuhimu wa kuelewa maisha ya mtoto mchanga anapozaliwa hadi miaka mitano, kwa minajili ya maisha ya baadaye.

Kaunti ya Kiambu mnamo Alhamisi ilijumuisha waandishi wapatao 15 katika hafla ya kuwahamasisha kuhusu ulezi wa mtoto mchanga mara anapozaliwa hadi umri wa miaka mitano.

Mtaalamu wa afya wa Kaunti ya Kiambu Bi Rachael Ndung’u, alisema unyoyeshaji wa mtoto mchanga ni muhimu kwa miezi sita ya mwanzo hadi umri wa miaka miwili.

“Wakati huo ndipo akili ya mtoto hukua timamu ili kuleta mwendelezo wa mawazo yake ya hapo baadaye,” alifafanua Bi Ndung’u.

Alieleza kuwa waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kuangazia mengi kuhusu ulezi wa mtoto na jinsi anavyostahili kupewa malezi bora.

Aliwakosoa baadhi ya wanawake ambao hudai kuwa wamejaliwa tu maziwa kidogo.

“Ni vyema kuelewa ya kwamba hakuna wakati mwanamke atakuwa na maziwa kidogo ikiwa ananyonyesha mtoto wake jinsi inavyostahili. Iwapo utakatiza mpango wa kunyonyesha kila mara bila shaka maziwa yatapungua,” alifafanua Bi Ndung’u.

Aliwashauri wanawake wanaonyonyesha kuwa sio lazima kuzoea maziwa ya mkebe ama za dukani kwa sababu hayo ndiyo husababisha mtoto kupatwa na shida ya kuharisha, marathi mengine madogo mwilini.

Alisema cha muhimu ni kunyonyesha matiti ya mama kwa miaka miwili ili mwili wa mtoto uweze kuwa inavyostahili.

Alitoa changa moto kwa wasichana wanaopata watoto kuwa wasiwe wepesi kutumia maziwa ya dukani huku wakiwanyima watoto wao matiti.

Alisema asilimia ya wanawake wanaonyonyesha imeshuka kutoka asilimia 85 mwaka wa 2020 hadi 83 mwaka wa 2021.

Dkt Teresa Mwoma aliye pia mhadiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) anasema lishe bora ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto mchanga.

Alisema iwapo mtoto hatapata lishe bora, kuna uwezekano wa akili yake kukosa kuumbika jinsi ipasavyo.

Alitaja masomo ya chekechea kama mmojawapo wa msingi wa mtoto kwani “hutoa mwelekeo wa maisha yake.”

Alisema serikali za kaunti zina jukumu kubwa kuona ya kwamba zinaendesha maswala ya chekechea kwa umakinifu ili kunufaisha watoto wanaokua.

Aliwataka wazazi popote walipo wawe mstari wa mbele kuwalea watoto wao kwa makini na upendo.

You can share this post!

MAPISHI: Jinsi ya kupika katlesi tamu za samaki

Natembeya aagiza vituo vya pombe vifungwe kijijini Hodi Hodi