• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
NMG yatoa msaada wa vitabu na vifaa muhimu vya masomo kwa shule ya Masaku

NMG yatoa msaada wa vitabu na vifaa muhimu vya masomo kwa shule ya Masaku

NA SAMMY KIMATU

KAMPUNI ya Nation Media Group (NMG) ilitoa msaada wa vitabu kwa wanafunzi katika shule ya Masaku School for the Physically Disabled, katika kaunti ya Machakos.

Mkuu wa Kitengo cha Mauzo katika NMG, Bw Philbert Julai aliongoza wafanyakazi wa NMG katika kilele cha hafla hiyo katika ukumbi wa shule hiyo kumkabidhi mwalimu mkuu, Bw Ndeto Ndunda vitabu.

Katika hotuba yake, Bw Julai alisisitiza umuhimu wa elimu na mahitaji mengine kwa watoto walemavu katika jamii.

Bw Julai aliangazia jinsi magazeti ya NMG yameratibu kurasa kadhaa katika majarida ya kila Jumatatu kutengewa nafasi za masuala ya elimu kwa wanafunzi wa sekondari na shule za msingi marufy NIE.

“Katika gazeti la Taifa Leo kuna fursa nzuri ya wanafunzi kuandika Insha. Manufaa yake ni kukuza lugha ya Kiswahili na Fasihi. Faida nyingine ni kwamba kuna Sh50,000 za kushindaniwa. Kiasi fulani cha pesa hizo humwendea mwanafunzi huku kingine kikimwendea mwalimu na sehemu inayosalia huendea shule ya mwanafunzi,” Bw Julai akasema.

Bw Julai alitoa wito kwa mashirika, makampuni na wahisani kushirikiana na NMG kuwasaidia walio na mahitaji spesheli miongoni mwa wasiobahatika katika jamii.

Mwalimu mkuu, Bw Ndeto Ndunda alitoa wito kwa wazazi wanaoficha watoto wao kutokana na ulemavu kuwapeleka shuleni.

Aliongeza kwamba ulemavu sio kilema na kusema walemavu wanaweza kufanya mambo bora zaidi kuliko watu walio na viungo vyao vya mwili sawa.

Bw Ndunda alisema wana changamoto nyingi kama walimu wakuu shuleni spesheli akisema mgao unaotolewa na serikali kwa shule zilizo na mahitaji spesheli hautoshelezi mahitaji yao.

“Mgao tunaopatiwa kwa shule za watoto walio na mahitaji spesheli ni kiasi kidogo. Wazazi nao wamelemewa na mzigo wa pesa kutokana na mfumko wa bei ya bidhaa nchini,” Bw Ndunda akaambia Taifa Leo.

Mwanachama wa bodi shuleni humo, aliye kadhalika daktari wa Therapia katika Hospitali ya Machakos Level Five, Bi Consolata Mwabu alisema washikadau wanapiga kampeni kubadilisha jina ‘Walemavu’ na kutafuta jina badala litakaloashiria maana nyingine.

Alisema waathiriwa huwa na unyanyapaa kutokana na jina ‘walemavu’.

Isitoshe, alisema shule hiyo ina uhaba wa ardhi akifafanua kwamba watoto walemavu hutakiwa kuwa na mazingira yanayokidhi mahitaji yao.

Dkt Mwabu liongeza kwamba Utafiti ulifanywa kati ya mwaka wa 2019 hadi 2020 na Wizara ya afya kwa msaada wa ufadhili kutoka kwa mpango wa Clinton Health Access.

Lengo la utafiti lilikuwa kubaini kiwango cha vituo vya kutoa huduma kwa walemavu nchini kenya. Ulifanyika katika hospitali 238 za kiwango cha Level  5 na 4 nchini kenya na hii ilihusisha kaunti 47. Miongoni mwa matokeo ya uchuguzi huo ulibaini kwamba angalau Wakenya 150,000 wanahitaji viti vya magurudumu na vifaa vingine vya kusaidia.

Hata hivyo ripoti iliyotolewa ilionesha ni asilimia 5 pekee kati yao wanaweza kumudu viti vya magurudumu vinavyofaa au wanoweza kupata kifaa vingine vinaowafaa walemavu.

Ripoti hiyo, akaongeza Bi Mwabu ilisema uhaba na ukosefu huo unatokanana na bei ghali ya vifaa.

“Chumba chetu cha watoto kufanyishwa mazoezi ya viungo kimekosa vifaa vinavyotakikana. Tukijaliwa kupata ufadhili, tutashukuru sana. Milango yetu iko wazi kwa kila mtu aliye na mwito wa kusaidia,” Dkt Consolata akasema.

Vilevile, aliongeza kwamba idadi ya walimu kwa wanafunzi ni ndogo zaidi.

Bali na shule hiyo kuwa ya walemavu, kuna wenzao chini ya 30 walio wanafunzi wa kawaida.

“Wale watoto wasio walemavu ni ndugu za walio walemavu. Wazazi huona heri wakisomea wote hapa kuliko kupelekwa shule mbalimbali,” Dkt Consolata akaongeza.

Shule hiyo ilainzishwa mwaka 1989 japo wanafunzi wa kwanza kusomea hapo ni wa darasa la mwaka 1985.

Kulingana na usimamizi wa shule, wanahudumia watoto kutoka PP1 hadi darasa la nane.

Kadhalika, matokea ya mitihani ya KCPE yaliyobadikwa katika ubao yanaonesha watoto katika shule hiyo hufanya vyema.

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi kufanyia kazi katika eneo lenye kelele

LSK yawataka wabunge kuwakataa ‘mawaziri’ wenye...

T L