• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Mudavadi kufanyia kazi katika eneo lenye kelele

Mudavadi kufanyia kazi katika eneo lenye kelele

NA MWANDISH WETU

HUENDA kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi akawa afisa wa cheo cha juu serikalini kuhudumu katika mazingira magumu zaidi baada ya kutengewa afisi katika jengo lililoko nje ya eneo la kifahari la afisi muhimu za serikali.

Mnamo Alhamisi, Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua alisema kwamba, afisi za Mkuu wa Mawaziri, wadhifa aliotengewa Bw Mudavadi katika serikali ya Kenya Kwanza, zitakuwa katika makao makuu ya Shirika la Reli la Kenya kwenye barabara yenye shughuli nyingi ya Haile Selassie, Nairobi.

Awali, kulikuwa na habari kwamba, Bw Mudavadi angekuwa na afisi katika jengo la Harambee House Annex, kunakopatikana afisi za Naibu Rais Rigathi Gachagua kwenye barabara ya Harambee Avenue ambapo kuna majengo ya kifahari yaliyo na afisi za serikali.

Haikubainika ni kwa nini Bw Mudavadi, ambaye kulingana na majukumu yake, atakuwa wa tatu katika mpangilio wa mamlaka katika serikali Kenya Kwanza, alitengewa afisi katika jengo linalopatikana hatua chache kutoka mtaa wa mabanda wa Land Mawe na karibu na kituo cha matatu zinazotoa kelele za kila aina cha Railways.

Barabara ya Haile Sellasie ni miongoni mwa zinazofahamika kwa msongamano wa magari jijini Nairobi, hasa katika mzunguko ulio kwenye makutano ya barabara ya Moi Avenue, na kwa kiongozi wa cheo cha Bw Mudavadi kuwa na afisi eneo hilo, ni vigumu kuepuka kuchelewa kuhudhuria mikutano nje ya afisi.

Ingawa serikali iko na majengo mengi ya kisasa katika barabara ya Harambee, katikati ya jiji, Community na Upper Hill, Bw Mudavadi ambaye majukumu yake yatamhitaji kufanya mikutano na maafisa wa wizara tofauti, kutengewa afisi katika jumba lililojengwa mnamo 1924 kunaweza kutatiza shughuli zake.

Tofauti na maafisa wengine wa serikali wakiwemo mawaziri anaopaswa kushirikisha ambao walitengewa afisi katika majengo yaliyo maeneo tulivu, Bw Mudavadi atalazimika kuvumilia kelele za manamba wa matatu na magari yao nje ya afisi zake.

“Haileti shangwe kupeleka Bw Mudavadi nje ya majumba ya kifahari kisha asemekane kuwa wa tatu kwa cheo katika serikali ya Kenya Kwanza,” alisema Francis Kavoo mkazi wa jiji la Nairobi.

Katika serikali ya Kenya Kwanza, Bw Mudavadi amemtwika jukumu la kumsaidia Rais na Naibu Rais katika kushirikisha na kusimamia Wizara na Idara za serikali.

Majukumu yake mengine ni kushirikisha ajenda ya kisheria ya serikali ya kitaifa katika wizara zote, kusimamia kamati za makatibu wa wizara na kutekeleza majukumu mengine ambayo atatengewa na Rais.

“Hapa itabidi MaDVD (Mudavadi) azoee kelele kutoka kwa matatu, manamba na magari ya moshi na raia wakienda nyumbani Landimawe,” alisema dereva wa matatu Oscar Kamau.

  • Tags

You can share this post!

Haji abadili nia kuhusu kesi ya gavana mstaafu

NMG yatoa msaada wa vitabu na vifaa muhimu vya masomo kwa...

T L