• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 8:55 AM
Nyanya aomba mahakama isimwachilie mwanawe jela

Nyanya aomba mahakama isimwachilie mwanawe jela

Na TITUS OMINDE

NYANYA ambaye mtoto wake amehukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kutishia kumuua, Ijumaa aliomba mahakama ya Eldoret isimwachilie akisema anahofia atamuua akitoka gerezani.

Teresia Ng’eno, 82, aliambia mahakama kuwa usumbufu kutoka kwa mwanawe, ambaye amekuwa akitishia kumuua mara kwa mara, umemfanya kuwa na hofu kuwa atamuua iwapo ataachiliwa akiwa angali hai.

Bi Ng’eno, ambaye alipinga vikali wazo la mwanawe kupewa kifungo cha nje, aliambia korti kuwa mara ya mwisho aliposhambuliwa na mtoto karibu akate roho.

Alimwambia Hakimu Mwandamizi wa Eldoret Naomi Wairimu kuwa kama majirani hawangeingilia kumnusuru siku ya tukio hilo, angekuwa marehemu.

Mlalamishi, ambaye alitokwa na machozi kortini alipokuwa akisimulia korti uchungu ambao mtoto wake wa tatu wa kiume amekuwa akimpa, alisema atakufa iwapo mkosaji ataachiliwa huru.

“Ikiwa korti hii itamwachilia huyu mtoto arudi nyumbani, hakika ataninua iwe kwa kunipiga ama kutokana na msukumo wa damu punde ninapomuona,” aliambia mahakama.

Ripoti ya maafisa wa probesheni ambayo iliwasilishwa mahakamani pia ilipinga mshtakiwa kupewa kifungo cha nje.

Kutokana na ripoti hiyo na ushahidi ambao uliwasislishwa kortini, mshtakiwa alitajwa kama mtundu na mhalifu tangu utoto wake.

Mzee wa kijiji cha eneo hilo Henry Ruto, ambaye alihojiwa na maafisa wa kerekebisha tabia, alimtaja kijana huyo kama mtu ambaye ni mtundu na msumbufu haswa wakati amelewa.

Bw Ruto alisema ameshughulikia visa kadhaa vya utovu wa nidhamu dhidi ya mkosaji katika afisi ya chifu wa eneo hilo, lakini kijana huyo amekataa kubadilika.

“Kijana huyu aliwahi kukamatwa na chifu alipojaribu kumbaka jirani yake. Ana kesi kadhaa za utovu wa nidhamu. Amekuwa akitishia wanakijiji wengine,” ilisema ripoti ya maafisa wa kurekebisha tabia iliyowasilishwa kortini.

Anatuhumiwa kumtishia kumuua mama yake nyumbani kwake katika eneo la Nainyei, katika Kaunti Ndogo ya Soy, Kaunti ya Uasin Gishu.

Mshtakiwa hakuonyesha kujutia makosa yake mbali alimlaumu mamake na dadake kwa kuchangia katika masaibu yake. Alidai kuwa mamake pamoja na dadake hawakumsaidia kuendelea na masomo katika chuo kikuu baada ya kufanya mtihani wa KCSE katika shule ya upili ya Chebar na kupata alama ya B.

Mahakama iliamua kumfunga jela miaka mitano.

  • Tags

You can share this post!

Rais akiri wanasiasa waeneza Covid

Chanjo: Rais aondoa hofu kuhusu AstraZeneca