• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Nyaribo kusalia gavana baada ya kura ya kumng’atua kuanguka

Nyaribo kusalia gavana baada ya kura ya kumng’atua kuanguka

NA WYCLIFFE NYABERI 

Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo ameponea hoja iliyolenga kumng’atua afisini.

Hii ni baada ya hoja hiyo kukosa kufikisha kigezo cha thuluthi mbili kama inavyohitajika kisheria ndiposa ang’atuliwe.

Kwenye kura iliyopigwa bungeni, madiwani 18 walipinga kung’atuliwa kwa Nyaribo ilhali 16 waliunga mkono hoja hiyo.

Ikiwa Nyaribo angeng’atuliwa, ni sharti kura za kuunga hoja hiyo zingefika 23.

“Kwa kuwa kigezo cha thuluthi mbili inavyohitajika kisheria hakikuafikiwa, hoja hii imeanguka,” akasema Spika Enock Okero.

Sababu 12 za kumng’atua kiongozi huyo wa chama cha United Progressive Alliance (UPA) zilikuwa zimeibuliwa.

Miongoni mwa sababu zilikuwa madai kwamba gavana huyo alitumia mamlaka yake vibaya, kutotii maagizo ya mahakama na kuajiri jamaa wake wa karibu katika nyadhfa moja kuu serikalini.

Diwani wa Esise, Bw Josiah Mang’era ndiye aliyewasilisha hoja ya kumbandua Nyaribo afisini.

Aliungwa mkono na diwani wa Kiabonyoru Minda Riechi.

Uongozi wa chama cha UPA uliwataka madiwani wake walioko bungeni Nyamira kuuangusha hoja hiyo iliyomweka Nyaribo mashakani.

Katibu mkuu wa chama hicho, chenye nembo ya pikipiki Jacob Bagaka, aliwaandikia madiwani hao waraka akisema kama chama hawaungi mkono gavana Nyaribo ang’atuliwe afisini.

Katibu huyo ambaye ni diwani katika gatuzi jirani la Kisii, alionya kuwa watakaoenda kinyume na agizo hilo watachukuliwa hatua za kinidhamu.

“Atakayekiuka uamuzi wa uongozi wa chama atasawiriwa kuwa msaliti. Hivyo ataweza kuadhibiwa vilivyo kwa mujibu wa sera za chama,” Katibu Mkuu alisema.

Mzozo kati ya madiwani na gavana Nyaribo ulitokota pale kiongozi huyo wa chama cha United Progressive Alliance (UPA) alimfuta kazi Waziri wake wa Afya Timothy Ombati.

Bw Nyaribo alisema Bw Ombati alikuwa amehusika kwenye ufujaji wa pesa zilizohitajika kwenye ununuzi wa dawa hospitalini.

Alidai waziri huyo alimhadaa kuzindua maboksi tupu ambayo hayakuwa na dawa ndani.

Hata hivyo, Bw Ombati alikana madai hayo.

  • Tags

You can share this post!

Sekta ya kahawa yayumba licha ya mageuzi na ahadi nyingi

Weledi wa demu wangu chumbani umenitia wasiwasi

T L