• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 10:59 AM
Ogier huyo! aongoza timu ya Toyota kunyakua nafasi za kwanza

Ogier huyo! aongoza timu ya Toyota kunyakua nafasi za kwanza

SUPASTAA Sebastien Ogier aliongoza wenzake kutoka timu ya Toyota kufagia nafasi tatu za kwanza katika siku ya kwanza ya Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally katika kituo cha kimataifa cha michezo cha Kasarani jijini Nairobi, jana.

Bingwa huyo mara saba wa dunia, ambaye anatetea taji lake la dunia na pia kuongoza msimu huu baada ya duru tano za kwanza, alikamilisha umbali wa kilomita 4.84 kwa dakika tatu na sekunde 21.5.Mfaransa huyo alimaliza sekunde 0.3 mbele ya raia wa Finland, Kalle Rovanpera (3:21.8) naye Muingereza Elfyn Evans akaandikisha 3:21.12.

Watatu hao wanaendesha magari ya aina ya Toyota Yaris.Ott Tanak kutoka Estonia na Mbelgiji Thierry Neuville wanaoendesha magari ya Hyundai, walifuatana katika nafasi ya tatu na nne, mtawalia. Bingwa wa dunia 2019 Tanak ataanza siku ya pili leo akiwa sekunde 2.5 nyuma ya kiongozi Ogier aliyefurahia kutawala mkondo wa kwanza kwa kasi Kasarani.

“Kesho (leo) ni mwanzo mkubwa wa mashindano haya. Inafurahisha kuona halaiki hii ya mashabiki. Kufikia sasa, naweza kusema mambo yangu yameniendea vizuri, ingawa kibarua kamili kitaanza kesho (leo),” alisema.

Itakumbukwa kuwa bingwa huyo wa mataji saba ya dunia pia ndiye alikuwa na kasi bora kuliko wote walioshiriki katika “shakedown” iliyojumuisha kilomita 5.15 katika mkondo wa Loldia katika eneo la Naivasha.Rais Uhuru Kenyatta alianzisha duru hiyo ya sita ya WRC nje ya Jumba la Mikutano la KICC katikati mwa jiji la Nairobi.

Inarejea kwenye WRC tangu 2002.Imevutia madereva 58. Kutoka KICC, madereva walielekea Kasarani saa nane kufanya mkondo huo maalum.Rais Kenyatta aliandamana na rais wa Shirikisho la Mbio za Magari Duniani (FIA) Jean Todt, Waziri wa Michezo Amina Mohamed na Afisa Mkuu Mtendaji wa WRC Safari Rally Phineas Kimathi, miongoni mwa wageni wengine.

Oliver Solberg, ambaye pia anaendesha mashine ya Hyundai i20, alifurahia kuwa bado mashindanoni. Gari lake liliharibika Juni 23 akifanya majaribio ya Safari Rally na kurekebishwa Jumatano.Hapo jana, raia wa Poland, Sobieslaw Zasada aliandikisha historia kwa kuwa dereva mzee duniani kushiriki duru ya WRC.

Zasada,91, alishiriki Safari Rally mwaka 1997 na kumaliza wa 12. Leo, madereva watafanya mikondo ya Chui Lodge (kilomita 13.34), Kedong (32.68km) na Oserian (18.87km) itakayorudiwa kufikisha jumla ya kilomita 129.78. Duru hiyo itaendelea Jumamosi kabla ya kufikia kilele Jumapili. Mashindano haya yanajumuisha kilomita 320.19.

  • Tags

You can share this post!

Kananu gavana wa 4 wa kike, Sonko akila hu kortini

Hisia kali zazidi kuibuka kuhusu Kieleweke 5 kuhamia UDA