• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Papa sasa atua Sudan Kusini kutafuta amani

Papa sasa atua Sudan Kusini kutafuta amani

NA MASHIRIKA

KINSHASA, DRC CONGO

PAPA Francis jana Ijumaa alikamilisha ziara yake ya kipekee katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuelekea katika nchi jirani ya Sudan Kusini, inayokumbwa na umaskini na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Matatizo yanayolikumba taifa hilo yaliendelea licha ya uwepo wake barani Afrika, baada ya watu 27 kuuawa katika jimbo la Central Equatorial Jumatatu, kwenye vita baina ya wachungaji na wanamgambo.

Papa alitarajiwa kuwasili nchini humo hapo jana, ambapo amepangiwa kuendeleza mchakato wa pamoja wa amani unaolenga kumaliza vita hivyo ambavyo vimedumu zaidi ya mwongo mmoja.

Hii ni ziara ya tatu ya Papa Francis, 86, kufanya barani Afrika tangu kuanza kuhudumu kama kiongozi wa Kanisa Katoliki mnamo 2013.

Alipowasili Jumanne katika jiji kuu la DRC, Kinshasa, alipokelewa kwa furaha na umati mkubwa wa watu wenye furaha. Hata hivyo, alikabiliwa na ukweli mchungu kuhusu athari za vita, umaskini na njaa.

Mnamo Jumatano, alielezwa simulizi za kusikitisha kutoka kwa waathiriwa wa vita, hasa katika eneo la mashariki mwa DRC, ambapo wengi wao wameshuhudia mauaji ya jamaa zao wa karibu, kulazimishwa kushiriki vitendo vya ngono, kukatwa sehemu za miili yao au kulazimishwa kula nyama za watu. Kiongozi huyo alikashifu vitendo hivyo, huku akitoa wito kwa pande zote husika—zilizo ndani na nje ya taifa hilo—ambazo zimekuwa zikijitajirisha kutokana na rasilimali asilia za nchini humo “kukoma kujifaidi kwa fedha zinazotokana na umwagikaji wa damu.”

Eneo la Mashariki mwa DRC Congo limekuwa likikumbwa na mapigano yanayotokana na mizozo inayoendelea kuhusu udhibiti wa madini muhimu kama vile almasi, dhahabu kati ya mengine ya thamani. Mizozo hiyo imekuwa ikiendelea baina ya serikali, wanamgambo na wavamizi kutoka mataifa jirani.

Tofauti baina ya DRC na Rwanda tangu mauaji ya kimbari nchini Rwanda mnamo 1994 pia yametajwa kuchangia mzozo huo.

Kwenye ujumbe wake, Papa Francis alisisitiza kuhusu umuhimu wa amani, akisema kuwa raia wa taifa hilo wanafaa kubaini kuwa maisha ya watu yana umuhimu mkubwa kuliko madini.

Papa aliondoka jijini Kinshasa jana Ijumaa baada ya kukutana maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini humo, ambapo baadaye alielekea jijini Juba, Sudan Kusini.

Katika ziara yake nchini Sudan Kusini, baadhi ya watu watakaojiunga naye ni Askofu wa Canterbury Justin Welby, ambaye ndiye kiongozi wa Kanisa la Kianglikana kote duniani. Pia, kiongozi mwingine wa hadhi ya juu atakayejiunga naye ni Iain Greenshields, aliye kiongozi wa Kanisa la Scotland.

Hiyo ndiyo ziara ya kwanza ya pamoja ya viongozi hao watatu, ambapo wameitaja kama “ziara ya amani.”

Welby alisema ameshtushwa na msururu wa mauaji uliofanyika siku moja kabla ya Papa kuwasili nchini DRC Congo.

  • Tags

You can share this post!

Aubameyang nje ya kikosi kitakachotegemewa na Chelsea...

TAHARIRI: Namwamba, viongozi nchini wasaidie klabu za soka...

T L