• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Pasta akiri kuwapachika mabinti wake wawili mimba

Pasta akiri kuwapachika mabinti wake wawili mimba

Na GEORGE MUNENE

MHUBIRI katika Kaunti ya Kirinyaga jana Jumanne alikiri kuwanajisi na kuwapachika mimba mabinti wake wawili walio chini ya umri wa miaka 18.

Mwanamume huyo alishtakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Anthony Mwicigi wa Mahakama ya Baricho kwa kutenda makosa hayo tarehe tofauti kati ya Juni 2019 na Agosti 2020 katika kijiji cha Kinyakiiru, eneobunge la Ndia.

Aliposomewa mashtaka, mhubiri huyo mwenye umri wa miaka 51 alikiri kuwa alishiriki ngono na mabinti wake ambao wana umri wa miaka 14 na 16.

“Ni kweli kwamba nilishiriki ngono na mabinti wangu,” akasema aliposomewa mashtaka na karani wa korti huku waliokuwemo wakiachwa vinywa wazi.

Kiongozi wa mashtaka Patrick Gikunju, aliomba korti kumzuilia mhubiri huyo ili kumpa wakati wa kupata cheti cha kuzaliwa cha watoto hao ili kuthibitisha umri wao kamili kabla hukumu haijatolewa.

“Bado hatujapokezwa cheti cha kuzaliwa cha watoto hao ambacho kinahitajika katika kudhibitisha umri kamili wa wasichana hao. Tunahitaji muda wa kupata stakabadhi hizo,” Bw Gikunju akaeleza korti.

Hakimu alikubali ombi la kiongozi wa mashtaka na akaamuru mhubiri huyo arejeshwe katika kituo cha polisi cha Sagana hadi Januari 7, ili stakabadhi hitajika ziwasilishwe kortini.

Aliongeza kuwa kufikia wakati huo mhubiri huyo atakuwa ametafakari kuhusu kukiri kwake kuwa alitenda makosa hayo.

Mhubiri huyo alikuwa ametoweka tangu mwaka jana na majuzi alikamatwa katika eneo la Mbeere Kusini kisha akazuiliwa katika kituo cha polisi cha Sagana alikohojiwa kuhusu madai ya kunajisi binti zake.

Habari zilisema alitoroka baada ya kugundua kuwa polisi walikuwa wakimsaka kuhusiana na kitendo chake cha kuwanajisi na kuwapachika wanawe mimba.

Mmoja wa mabinti hao tayari amejifungua huku mwingine akiwa na mimba ya miezi saba.

Hivi majuzi, wabunge wawakilishi wawili, Wangui Ngirici (Kirinyaga) na Gladys Shollei (Uasin Gishu) waliandaa maandamano wakitaka mhubiri huyo akamatwe na ashtakiwe.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA AFYA: Ugonjwa wa ‘kusikia sauti kichwani’...

Jubilee na ODM njia panda kuhusu uchaguzi mdogo wa ugavana...