• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
SHINA LA AFYA: Ugonjwa wa ‘kusikia sauti kichwani’ nusura umharibie maisha

SHINA LA AFYA: Ugonjwa wa ‘kusikia sauti kichwani’ nusura umharibie maisha

Na PAULINE ONGAJI

ALIPOGUNDULIKA kuwa na maradhi ya akili, nusura maisha yake yafikie kikomo kwani hali hii ilisitisha taaluma na masomo yake.

Masaibu ya Kenneth Nzioka, 33, yalianza mwaka wa 2015 alipogundulika kuwa na maradhi ya Paranoid Schizophrenia, ugonjwa wa akili unaomsababisha mgonjwa kukumbwa na fikra zisizoambatana na matukio halisi.

Wakati huo Nzioka alikuwa mwanafunzi katika Chuo cha Berlin School of Economics, jijini Berlin, nchini Ujerumani. Aidha, alikuwa akifanya kazi katika shirika moja la kifedha jijini humo.

Maradhi yake yalianza kama sauti kadhaa zilizotawala fikra zake na zilizokuwa zikimzungumzia.

“Mwanzoni nilizipuuza lakini sauti hizo ziliendelea kunisemesha. Zingeniambia kuhusu mambo mabaya. Wakati mwingine zilinikumbusha mambo niliyofanya kale, vile vile mambo mabaya kuhusu watu walio karibu nami,” aeleza.

Kwa mfano, asema, sauti hizi zingemwambia “hebu mwangalie yule, usile kile, mamako amefanya hili au lile.”

Mambo yaliendelea kuwa mabaya sana kiasi cha kuwa sasa alianza kufuata chochote ambacho sauti hizi zingemwelezea. Hali hii pia ilimuathiri sio tu kifedha au kijamii, bali pia kitaaluma.

“Kazini ningekaa pembeni na kujitenga kwa sababu sikumwamini yeyote. Shuleni, sauti hizi hata zingenipa majibu kwenye mtihani, suala lililoathiri sana masomo yangu,” aongeza.

Kwa hivyo alilazimika kuacha kazi na masomo na kurejea humu nchini angalau pengine kuidhibiti hali hii. Na aliporejea humu nchini mwaka wa 2017, hali ilikuwa mbaya zaidi. Athari za maradhi haya ziliendelea kujitokeza na hata kumkosanisha na baadhi ya jamaa zake, waliohusisha hali hii na ushirikina.

“Kuna nyakati ambapo ningefanya vituko kwa kupiga mayowe, kutoroka, au kuingia kwenye basi na kusafiri mbali pasipo kujua nilipokuwa naelekea,” asema.

Alilazimika kupokea matibabu ya kisaikolojia.

“Nilihudhuria vikao kadha wa kadha vya tiba ya kisaikolojia katika idara ya matibabu ya kiakili katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.”

Hata hivyo, baada ya muda hangeweza kuendelea kumudu gharama ya kimatibabu na hivyo akasitisha.

Kando na hayo, mara kadhaa alipelekwa kwa lazima katika hospitali ya kiakili ya Mathari.

“Nilipelekwa katika hospitali hii mara tatu ambapo wakati wa kwanza nilidungwa sindano na kipewa dawa kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.”

Hata hivyo, Januari mwaka jana, Bw Nzioka asema, hali yake iliimarika baada ya sauti hizo kutoweka. Hii ilikuwa mara ya pili kwake kupata nafuu kwani mwezi Januari mwaka wa 2019 sauti hizo zilitoweka, lakini zikarejea miezi michache baadaye.

Kwa sasa Nzioka anasema kwamba hali yake imeimarika.

“Nilimuona daktari mwisho wa mwezi Novemba mwaka 2019 katika hospitali ya kiakili ya Mathari. Sikupewa dawa, bali nilipendekezewa matibabu ya kisaikolojia na ushuari nasaha.”

Kulingana na Dkt Marx Okonji, daktari wa akili jijini Nairobi, schizophrenia ni maradhi ya akili inayoathiri fikra, hisia na tabia za mtu.

Mwunganisho wa kijenetiki

Ni hali ambayo husababishwa na masuala mbali mbali, lakini hasa hutokana na mwunganisho wa kijenetiki.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba katika familia za wanaokumbwa na hali hii kuna jamaa ambaye anayo au amewahi kuwa na matatizo ya kiakili,” aeleza.

Maradhi haya yanayoathiri 1% ya watu ulimwenguni kote huambatana na ishara kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na mhusika kutoonekana kukubali uhalisi wa maisha.

“Aidha, mwathiriwa ataanza kukumbwa na matatizo ya kuzungumza, kupunguza ushiriki katika shughuli za kawaida na kukosa kumakinika katika mambo ambayo awali yalimfurahisha,” aeleza.

Dkt Okonji asema ni kibarua kwa maradhi haya kutambuliwa kwa urahisi kwani ishara zake hazijitokezi haraka.

“Watu wengi wanaougua maradhi haya huendelea na shughuli zao za kawaida. Utawaona wakivalia vyema, wakisoma na hata kufanya kazi kama kawaida,” aeleza.

Kuanzia umri wa kubaleghe

Aina moja ya schizophrenia, asema, hujitokeza wakati wowote kuanzia umri wa miaka ya kubaleghe, hadi miaka 18.

“Kuanzia hapo mwathiriwa ataanza kuonyesha tabia zisizo za kawaida. Kama ni masomo, yatarudi chini, huku pia uhusiano na wenzake ukiathirika pakubwa kwani ataanza kujitenga,” aeleza.

Kujitenga huku hutokana na hisia zisizo za kawaida na za kweli kuhusu mazingira ya mwathiriwa.

“Hisia hizi hutokana na sauti ambazo mwathiriwa anasikia. Kwa mfano, atasikia sauti za watu wakimsema au wakimzungumzia kwa kawaida. Hapa mwathiriwa atashuhudiwa akiwazungumzia na hata kujaribu kujibu sauti za watu hawa wasioonekana. Pia, ni kawaida kwa mwathiriwa huanza kupuuza shughuli za kawaida kama vile kudumisha usafi,” aeleza.

Kulingana na Dkt Okonji, kuna aina nyingine ya maradhi haya ambayo hukumba watu kuanzia miaka 30.

“Huyu ni mtu ambaye alikuwa akiendelea vyema kimaisha, lakini ghafla anaanza kuamini sauti na mambo yasiyokuwepo. Kwa mfano utampata mwathiriwa akijiita Yesu. Akili zao ni timamu lakini wanaamini mambo yasiyokuwa ya kawaida.”

Mbali na mwathiriwa, Dkt Okonji anasema kwamba, jamaa na familia za mhusika pia huanza kushuhudia athari za hali hii.

“Kumbuka huyu ni mtu ambaye kwa viwango vya kawaida, alikuwa sawa na hata alikuwa akifanya vyema kimaisha, lakini sasa ghafla ameanza kufanya mambo ya kushangaza,” aeleza.

Ni hapa ndipo kunatokea hatari ya mwathiriwa kuanza kupata shinikizo la kupokea matibabu tofauti yasiyoambatana na maradhi haya, na hivyo kufanya hali yake kuwa mbaya hata zaidi. Ndiposa mtaalamu huyu anasisitiza kwamba utambuzi na matibabu ya kitaalamu utahitajika.

“Japo maradhi haya hayana tiba, kuna mbinu za kimatibabu za kudhibiti hali hii. Kwa wale ambao wamethibitishwa kuwa wanaugua schizophrenia, daktari atapendekeza dawa tunazoziita anti-psychotic drugs zinazopunguza hisia hizi zisizo za kawaida,” asema Dkt Okonji.

Kwa kawaida, anaongeza kwamba, pindi maradhi haya yametambulika, asilimia 25% ya waathiriwa wanaopokea matibabu watapata nafuu, lakini lazima waendelee kupokea matibabu. Aidha, asilimia 25% ya waathiriwa watapata nafuu kwa viwango fulani, lakini hawatorejelea hali ya kawaida kikamilifu.

“Asilimia 25 ingine ya wagonjwa hawatapata nafuu kamwe, na ndiposa nasisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia dawa. Asilimia nyingine 25 wataamini kwamba wamepona kabisa, na huo ni uwongo kwani maradhi haya hayana tiba bali yanadhibitiwa tu.”

Kwa wale ambao huenda baadaye watajitokeza na kudai kwamba wamepona kabisa, Dkt Okonji asema, kuna uwezekano mkubwa kwamba mwanzoni utambuzi wa maradhi hayo ulikuwa wa kimakosa, au ishara zilikuwa athari za hali nyingine.

Kwa mfano, Dkt Okonji anasema kwamba kuna baadhi ya watu wanaokumbwa na ishara hizi kutokana na maradhi mengine ambayo huenda yakaathiri akili, kama vile malaria na homa kali.

“Pia, kuna wale ambao ishara hizi zaweza kutokana na matumizi ya mihadarati kama bangi, ambapo pindi mwathiriwa anapokoma kuzitumia, hali yake ya kawaida inarejea,” aeleza.

Hata hivyo, anasema kwamba kwa waathiriwa ambao wamethibitishwa kuugua maradhi haya na kuanza kupokea matibabu, kuna hatari ya hali yao kudorora baada ya muda.

“Mojawapo ya changamoto ni kwamba kwa wengi, ni kibarua kudumisha matumizi ya dawa hasa kwa wale wanaotumia tembe za kumezwa kila siku. Ndiposa tunapendekeza matumizi ya dawa zinazotumiwa mara moja baada ya mwezi mmoja au miezi kadhaa kwani inakuwa rahisi kwa mwathiriwa kufuatilia ratiba, na hivyo kuzuia tatizo la maradhi haya kuchipuka tena baada ya kudhibitiwa,” aeleza.

Anaongeza kwamba changamoto nyingine kuu ni kwa waathiriwa kukubali hali yao.

“Kuna baadhi ya waathiriwa ambao kamwe hawaamini kwamba wana maradhi ya akili. Ndiposa utakumbana na baadhi yao wanaosisitiza kwamba baada ya muda wamepona ilhali hali hii haina tiba,” aeleza.

“Wakati mwingine ni vyema kwa mwathiriwa kushauriwa ili ajue na kukubali kwamba atahitajika kutumia dawa kwa muda mrefu, na kwamba hili sio jambo la kumfanya aone aibu.”

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Barua kwa Rais: Kang’ata aomba msamaha

Pasta akiri kuwapachika mabinti wake wawili mimba