• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Pesa zaleta mpasuko katika Baraza la Wazee wa Njuri Ncheke

Pesa zaleta mpasuko katika Baraza la Wazee wa Njuri Ncheke

NA ALEX NJERU

BARAZA la wazee wa Njuri Ncheke katika Kaunti ya Tharaka Nithi limegawanyika mara mbili kufuatia mgogoro wa matumizi ya pesa.

Kundi moja linaongozwa na Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa wa baraza hilo Bw Alphonse Kamwara na lingine likiongozwa na Mwenyekiti wa tawi la Tharaka Bw Mbiti Rugiongo.

Kikundi cha Rugiongo kinadai Kamwara anatumia fedha za wazee bila kuwajulisha, tuhuma ambazo Kamwara amekanusha.

Wakihutubia wanahabari mjini Tharaka mnamo Jumatano, wazee wanaoegemea upande wa Rugiongo walimpa Kamwara siku 14 kutoa hesabu ya pesa zote zilizotumika na kama sivyo, watachukua hatua kwa mujibu wa taratibu za baraza hilo.

“Kamwara amekuwa akitumia pesa za baraza na marafiki wake wachache bila idhini ya wanachama na kila anapoulizwa kutoa hesabu za matumizi, anakataa,” alisema Bw Rugiongo.

Pia alimpiga marufuku Kamwara kusimamia shughuli za Njuri Ncheke katika eneobunge la Tharaka akidai kwamba anafaa kuhudumu katika afisi ya kitaifa pekee.

Aliongeza kuwa timu ya viongozi wanaoshirikiana na Bw Kamwara inapaswa kukabidhi uongozi kwa timu hiyo mpya mara moja.

Bw Mati Nkubitu, mzee mwingine, alisema Bw Kamwara amekuwa akiamuru shughuli za baraza hilo bila kuwahusisha viongozi wengine, shutuma ambazo amekanusha na kusema ni za uongo na kusisitiza kwamba ataendelea kuwa madarakani.

Bw Kamwara alisema ni wazee wachache wenye kiu ya madaraka ambao wamejitenga na baraza hilo na kwamba watashughulikiwa kwa kufuata taratibu.

Baraza la Njuri Ncheke hupata fedha zake kutoka kwa wafadhili, yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanawashirikisha katika kusukuma baadhi ya ajenda muhimu kwa jamii.

Wazee hao pia hupata ruzuku kutoka kwa viongozi, wakiwemo wanasiasa kwa ajili ya kufanya baadhi ya mazoezi kama vile kupanda miti.

  • Tags

You can share this post!

Sakaja apata shavu mpango wa ‘Dishi na County’...

Mbunge Samuel Atandi afurushwa bungeni kwa kudai Gachagua...

T L