• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Petanns yafungua chuo cha kiufundi kuwasaidia vijana kupata ujuzi

Petanns yafungua chuo cha kiufundi kuwasaidia vijana kupata ujuzi

NA LAWRENCE ONGARO

SHULE ya mafunzo ya udereva ya Petanns imebuni chuo cha kiufundi ili kuwasaidia vijana kupata ujuzi kamili.

Mkurugenzi wa Petanns Bw Peter Muinami, kwa kauli moja amewahimiza wazazi popote walipo walete vijana katika chuo hicho ili wapate ujuzi wa kutosha.

“Chuo hiki kwa muda mrefu kimekuwa mstari wa mbele kutoa masomo ya kuaminika yenye umuhimu katika soko la ajira. Kwa hivyo sioni maana yoyote vijana kuketi nyumbani bila kufanya lolote,” alifafanua mkurugenzi huyo.

Mwalimu mkuu wa chuo hicho Bi Susan Mwangi alisema wana matawi kadha katika maeneo tofauti hapa nchini.

Baadhi ya matawi hayo yapo Ruiru, Thika, Nakuru, Limuru, na Githurai.

Alisema chuo hicho kimejitolea mhanga kuona ya kwamba kozi muhimu zinazoendeshwa hapo ni udereva, urembo, upishi, maswala ya ushauri, uokaji wa mkate, na ujuzi wa umeme.

Baadhi ya wanafunzi wa Petanns. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Aliwahimiza wanafunzi ambao hawajapata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu kuchukua hatua ya kujiunga na maswala ya kiufundi.

“Katika siku zijazo kazi ya kiufundi itapata faida kubwa na kwa hivyo ni vyema vijana kuchukua hatua ya haraka na kujiunga na kozi ya kiufundi,” alieleza Bi Mwangi.

Alitoa wito kwa wazazi popote walipo hasa mjini Ruiru kuchukua jukumu la kupeleka wana wao kufanya kozi ya kiufundi ili wawe na nafasi ya kupata ajira.

Meneja wa chuo cha Petanns Bw Amos Muiruri, alisema chuo hicho kimebuni mbinu ya kufunza wanafunzi kazi ya udereva kikamilifu.

“Sisi tunajitolea mhanga kuona ya kwamba mwanafunzi anatoka chuoni huku na ujuzi kamili,” alisema  Bw Muiruri.

Alisema mbali na kufundishwa udereva wanafunzi wanapewa ujuzi wa huduma ya kwanza (First Aid), jinsi ya kurekebisha makosa madogo kwenye gari, na pia kuwa makini kabla ya kuendesha gari.

Alisema chuo hicho kina uwezo pia wa kuwatafutia kazi wanafunzi  baada ya kukamilisha masomo yao.

“Chuo hiki kinahakikisha kila mwanafunzi anafuzu kikamilifu ili akienda kutafuta ajira awe amekamilika kiujuzi,” alisema meneja huyo.

Mwanafunzi Teresina Wanjiru ambaye anasomea Diploma katika maswala ya hoteli, alitoa wito kwa vijana wanaokamilisha elimu ya shule kujiunga na kozi zitakazowafaidi kimaisha.

“Mimi ninatarajia kukamilisha kozi yangu hivi karibuni na kwa hivyo nina imani nitapata kazi  kutokana na ujuzi wangu,” alisema Wanjiru ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza.

Bw Dominic Muya anayesomea somo la mawasiliano anasema kila mwanafunzi anayefanya kozi yoyote ile ana nafasi nzuri ya kufanikiwa kimaisha.

“Vijana wanapokamilisha shule hawafai kuketi bure bali wanastahili kufanya kozi ya kiufundi,” alisema Bw Muya.

  • Tags

You can share this post!

Elimu: Trevor Osore, 15 aliyeangaziwa na magazeti ya NMG...

Putin awazia kutumia ‘silaha zisizo za kawaida’...

T L