• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Polisi amuua mpenzi wa pembeni aliyelazwa hospitalini

Polisi amuua mpenzi wa pembeni aliyelazwa hospitalini

Na STELLA CHERONO

WAKAZI katika eneo la Njoro, Kaunti ya Nakuru, walikumbwa na mshtuko baada ya afisa wa polisi kumwandama mpenziwe hadi hospitalini alimokuwa akitibiwa na kumuua kwa kummiminia risasi.

Konstebo Bernard Kivo kutoka Kituo cha Polisi cha Njoro aliingia ghafla katika Hospitali ya Njoro, akiwa amejihami kwa bunduki, na kumpiga risasi mara 13 mpenziwe Mary Nyambura, aliyefariki papo hapo.

Bi Nyambura alifika hospitalini mwendo wa saa tano usiku akiwa na majeraha kwenye mguu wake wa kulia kabla ya afisa huyo aliyevalia kiraia kuingia na kumwangamiza.

Kulingana na taarifa ya polisi iliyoonekana na Taifa Leo, Konstebo Kivo aliyekuwa kwenye zamu katika Kituo cha Polisi cha Njoro, aliwaarifu maafisa wenzake kwamba, alitaka kwenda kujibu simu nje ya kituo hicho kabla ya kumfuata mwanamke huyo anayeaminika kuwa mpenziwe hospitalini.

Alirejea kituoni baada ya kutekeleza mauaji hayo huku akionekana kutatizika na kufyatulia risasi kila kitu kiholela.

Wenzake walijaribu kumpokonya bunduki huku wakihofia maisha yao ambapo Bw Kitivo alipata fursa ya kujipiga risasi kidevuni na kujiua papo hapo.

Akizungumza na Taifa Leo jana, mke wake Konstebo Kivo, Joyce Ndunge, 29, aliyejawa na simanzi kufuatia tukio hilo alisema kwamba, hakuwa na habari kwamba mumewe waliyezaa naye watoto wawili alikuwa angali katika uhusiano na Bi Nyambura.

Alisema marehemu alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mumewe hapo awali lakini mumewe alikuwa amemweleza kuwa uhusiano huo ulikatika mwaka mmoja uliopita.

“Sikufahamu kwamba bado walikuwa pamoja. Tumekuwa tukizozana kuhusu suala hilo lakini alinihakikishia kwamba walikuwa wameachana. Nilishtuka nilipofahamu kwamba amemuua,” alisema Bi Ndunge.

Afisa huyo aliondoka kuelekea kazini mwendo wa saa tano usiku akiwa amevalia suruali ndefu aina ya jeans, shati kisha akavalia sare yake juu na korti na hakuonekana mwenye matatizo.

Hata hivyo, alipiga simu baada ya dakika kumi na kumwarifu mkewe kuwa amemuua mpenzi wake aliyesema amekuwa akijaribu kuharibu ndoa yao na kusema kwamba anapanga kujitoa uhai vilevile.

Baada ya kupokea simu hiyo, Bi Ndunge alielekea kituoni ili kujaribu kumtuliza bila kufua dafu.

Bi Nduge alifichua kuwa ndoa yao ya miaka saba ilikuwa na amani hadi Bi Nyambura alipojitokeza.

“Nimekuwa nikiwasiliana na msichana huyo kupitia WhatsApp, na wakati mwingine nikimpigia simu na kumsihi aache ndoa yangu kwa sababu alikuwa ameolewa vilevile hapo awali. Nilitaka tu kuokoa ndoa yangu,” alisema.

Madaktari katika hospitali alimouawa Bi Nyambura walisema aliletwa na mwendeshaji boda-boda na hakuwa amelazwa kwa sababu alikuwa anafanyiwa ukaguzi kwanza.

Bw Paul Karanja, mkazi aliyeishi karibu na duka la kuuza vileo ambapo Bi Nyambura alikuwa akifanya kazi alisema wawili hao wamekuwa na matatizo katika miezi miwili iliyopita na wakati mwingine wangepigana hadharani.

You can share this post!

Omondi kukosa Raga za Dunia mijini Vancouver na Edmonton...

ODONGO: Kifo cha BBI chaweka OKA hatarini zaidi 2022