• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
ODONGO: Kifo cha BBI chaweka OKA hatarini zaidi 2022

ODONGO: Kifo cha BBI chaweka OKA hatarini zaidi 2022

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI wa OKA wanafaa kughairi kiburi chao kisha wakimbilie muungano na Naibu Rais William Ruto au Kinara wa ODM Raila Odinga ili angalau kutwaa wadhifa wa mwaniaji mwenza, la sivyo watakaa kwenye baridi kisiasa kwa miaka mingine mitano.

Hatua ya mahakama ya rufaa ya kushikilia uamuzi wa mahakama kuu na kuzima Mpango wa Maridhiano (BBI) sasa unawaacha vinara wa OKA kwenye njiapanda zaidi kuelekea 2022.

Viongozi wa OKA Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi wa Kanu wasipoharakisha na kuenda kwenye ama kambi ya Dkt Ruto au Bw Odinga watajipata katika njia panda na kuzama kisiasa.

Hesabu za wanasiasa hawa zimekuwa zikiegemea sana kufaulu kwa BBI ambapo kungekuwa na nyadhifa kadhaa za juu ambazo wangemegewa.

BBI ilikuwa itenge nafasi za Waziri Mkuu na Naibu wake na si siri vinara hawa wa OKA walikuwa wakiotea nafasi hizo.

Kuhusiana na kauli yao ya kila mara kuwa wanalenga kuwania Urais, hiyo huenda ikawa ni kibarua kigumu kutokana na kukosa uungwaji mkono miongoni mwa wapigakura wakilinganishwa na Dkt Ruto na Bw Odinga

Hata kura kutoka ngome Mabw Mudavadi na Musyoka nazo zikiunganishwa hazitoshi kuwashindia urais kutokana na mgwanyiko wa kisasa Ukambani na Magharibi.

Mabw Wetang’ula na Moi nao hawana umaarufu wowote wa maana wa kuwawezesha kuwania kiti cha urais na wanaonekana tu kama wanaojitafutia nafasi katika serikali itakayobuniwa 2022.

Tayari kinara wa ODM Raila Odinga wikendi alitangaza kuwa sasa umakinifu wake ni kumenyana na Dkt Ruto 2022 debeni 2022 baada ya kuzama kwa BBI.

Hata hivyo, kushinda kiti cha Urais kunahitaji mgombeaji mwenza kutoka eneo ambalo lina wapiga kura wengi.

Hali ilivyo kwa sasa, huenda Dkt Ruto na Bw Odinga wote wananyemelea mwaniaji mwenza kutoka ukanda wa Mlima Kenya.

Dkt Ruto tayari ana uungwaji mkono mkubwa na umaarufu wake utapanda zaidi iwapo atakuwa na mwaniaji mwenza kutoka eneo hilo.

Hata hivyo, hilo huenda likazua mjadala kuwa maeneo ya Bonde la Ufa na Kati yanabadilisha nyadhifa za urais na makamu wake.

Rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta alimteua Daniel Moi kuwa makamu wake na alipoaga dunia 1978, Mzee Moi alimteua Mwai Kibaki kuwa makamu wa Rais.

Aidha Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto wameongoza pamoja na sehemu nyingine za nchi zitaonekana kutengwa iwapo Rais na Naibu wake watatoka Bonde la Ufa na Kati tena.

Hii ndio maana mmoja kati ya Mabw Musyoka na Mudavadi wanafaa kutathmini hali na kuamua kuwa mgombeaji mwenza wa Dkt Ruto au Bw Odinga kwa kuwa hakuna nyadhifa zozote za juu kuliko hizo chini ya katiba ya sasa.

Iwapo viongozi wa OKA wataafikiana na kuunga mkono mmoja wao basi kuna uwezekano wanaweza tu kuibukia nafasi ya tatu na kulazimisha duru ya pili ya uchaguzi.

You can share this post!

Polisi amuua mpenzi wa pembeni aliyelazwa hospitalini

Madiwani waasi ODM baada ya Kingi kuadhibiwa