• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Polisi kukamatwa kwa kutofika kortini

Polisi kukamatwa kwa kutofika kortini

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi katika kitengo cha polisi cha Flying Squad kilichovunjiliwa atakamatwa kwa kutofika kortini kutoa ushahidi katika kesi ya uvurugaji amani dhidi ya Mbunge wa zamani James Ndung’u Gethenji.

Bw Evans Murira aliagizwa akamatwe kisha afikishwe mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku kuchukuliwa hatua kali kwa kukaidi agizo la korti.

Bw Murira anayehudumu katika kituo cha Polisi cha Londiani anatarajiwa kufikishwa kortini Feburuari 22,2021 kabla ya kusikizwa kwa kesi dhidi ya Bw Gethenji na washtakiwa wengine sita.

Bi Mutuku alitoa agizo hilo kufuatia ombi la kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda. Bw Gikunda alieleza mahakama kuwa Bw Murira amepelekewa samanzi za kufika kortini kutoa ushahidi dhidi ya Bw Gethenji mara tatu lakini “akadinda”

Bw Gikunda aliomba mahakama itoe kibali cha kumtia nguvuni afisa huyo anayehudumu katika kitengo cha uchunguzi wa uhalifu (DCI).

Ombi hilo liliwashangaza mawakili Ishmael Nyaribo na Willis Otieno wanaomwakilisha Bw Gethenji. Akauliza Bw Nyaribo, “Je, kweli ukimleta shahidi umemtia pingu atakuwa huru kweli kutoa ushahidi kwa njia ya haki?”

Bw Gikunda alijibu akasema inabidi sasa Bw Murira akamatwe na kufikishwa kortini kutoa ushahidi kwa nguvu.

Bw Gikunda aliwasilisha ombi la kukamatwa kwa Bw Murira baada ya afisa mwingine wa polisi Konstebo Mwangi Njenga kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Konst Njenga alikabiliwa na wakati mgumu kujibu maswali kutoka kwa Mabw Nyaribo na Otieno alipotoa ushahidi dhidi ya Bw Gethenji.

Afisa huyo wa polisi anayehudumu katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) alisem kitengo cha Flying Squad alipohudumu kwa miaka mitano kilibuniwa kupambana na visa vikali vya uhalifu kama vile wizi wa mabavu.

Konst Mwangi alieleza mahakama mnamo Julai 2 2019 alipigiwa simu kuenda mtaa wa Kihingo Village kushughulikia kisa cha uhalifu.

Alisema mkubwa wake alipigiwa simu na wakili Prof George Wajackoya aliyeripoti kwamba ameshambuliwa pamoja na mteja wake Bw Kishor Kumar Varsani na wahuni mtaani humo.

Afisa huyo wa polisi alisema alifika pale na kuwapata afisa mkuu (OCS) kituo cha polisi cha Gigiri na afisa mkuu wa uchunguzi wa jinai eneo hilo (DCIO) katika mtaa wa Kihingo Village Waridi Gardens.

“Nilipofika Kihingo nilikuta Bw Gethenji na mkurugenzi mwenzake katika kampuni ya Kihingo Village Waridi Gardens Management One Limited iliyostawisha mtaa huo wa kifahari wa Kihingo ulio na thamani Sh20bn,” Konst Njenga.

Afisa huyo alisema Mabw Gethenji na Mabanga walikuwa ndani ya gari na “ilihofiwa walikuwa wanajaribu kutoroka.”

Akihojiwa na Mabw Otieno na Nyaribo afisa huyo alisema “hakushuhudia wawili hao wakizua vurugu na kuwashambulia Prof Wajackoya na Bw Varsani.”

Wakili Willis Otieno anayewakilisha Gethenji na washtakiwa wengine 6.

Shahidi huyo alieleza mahakama Alhamisi, punde tu alipofika Kihingo hakuona likiwa jambo la busara kuwashirikisha OCDP na DCIO wa Gigiri katika uchunguzi wake kwa vile ulikuwa unaendelezwa na kikosi cha Flying Squad.

“Je suala la kuzusha vurugu ni uhalifu mkali uliostahili kushughulikiwa na Flying Squad?” Bw Otieno alimwuliza Konst Njenga.

“Uhalifu ni uhalifu na hakuna ule usioweza kushughulikiwa ni kitengo chochote cha polisi,” alijibu.

“Ikiwa Flying Squad ilibuniwa kupambana na uhalifu mkali kama wizi wa mabavu na wizi wa magari.Kulikuwa na kisa chochote kama wizi wa mabavu ama wizi wa gari ulichoarifiwa kimetokea Kihingo?” Bw Nyaribo alimwuliza shahidi huyo.

“Hapana,” alijibu.

“Kwa hivyo ulienda Kihingo kutazama fulana ya Bw Varsani iliyokuwa imeruriwa katika purukushani hiyo. Je huku sio kutumia vibaya kikosi cha Flying Squad,” Bw Nyaribo.

Konst Njenga alisema aliagizwa na aliyekuwa mkubwa wangu Bw Musyoka aende Kihingo kuchunguza kilichoendelea.

Afisa huyo wa polisi alikarangwa kwa maswali mazito sababu kikosi cha Flying Squad kilitumwa kwa nyumba ya Bw Gethenji ilhali hakuwa amefanya uhalifu.

“Je wakati ulifika Kihingo ulimkuta Bw Gethenji kwa nyumba nambari 26D anamoishi Bw Varsani aliyelalamika amepigwa na wahuni na kuwafukuza mafundi waliokuwa wanajenga kwake?,” Bw Nyaribo alimwuliza Konst Njenga.

“Sikuwapa Bw Gethenji na Mabanga kwa Bw Varsani,” alijibu.

Aliendelea kusema hakuwapata washtakiwa wengine katika kesi hiyo Kihingo kwa vile walikuwa wametoroka.

Afisa huyo alisema aliyekuwa mkuu wa kitengo hicho cha Flying Squad Bw Musa Yego pia alifika Kihingo wakati wa zogo hilo.

“Unajua sababu za kukivunja kikosi cha Flying Squad?” Bw Nyaribo alimwuliza shahidi huyo. “Hapana sijui.Waliokivunja ndio wanajua. Hilo ni suala la usimamizi wa kikosi cha Polisi,” alisema.

Bw Nyaribo alimweleza sababu ya kuvunjwa kwa kikosi hicho ni kwasababu maafisa wake walikuwa wanatumia vibaya mamlaka yake.

Shahidi huyo alikana alikuwa na kisasi dhidi ya Gethenji na kuongeza “ alimwona mara ya kwanza siku hiyo.”

Kesi itaendelea Februari 23,2021

  • Tags

You can share this post!

Aliyejifanya Mhindi Facebook ashtakiwa kwa ubakaji

Shinikizo Ruto na Gideon Moi waungane