• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Shinikizo Ruto na Gideon Moi waungane

Shinikizo Ruto na Gideon Moi waungane

VALENTINE OBARA na FLORAH KOECH

VIONGOZI katika ukanda wa Bonde la Ufa wamewataka Naibu Rais Dkt William Ruto na Seneta wa Baringo Gideon Moi, kuweka kando tofauti zao za kisiasa.

Wawili hao wamekuwa wakivutana kwa muda mrefu kuhusu anayestahili kuwa kigogo mkuu wa kisiasa katika ukanda huo, ambao huwa na idadi kubwa ya wapigakura.

Kando na kuwa wote wawili wanaazimia kuwania urais mwaka 2022, wanatofautiana pia kuhusu marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kwa upande mmoja, Dkt Ruto anapinga mfumo utakaotumiwa kupiga kura hiyo ya maamuzi, ambayo inaungwa mkono kikamilifu na Seneta Moi.Jana katika mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti mkuu wa Benki ya Co-operative, Hosea Kiplagat, baadhi ya viongozi waliohudhuria waliwaambia wazi wawili hao kwamba tofauti zao ni kikwazo kwa umoja wa eneo hilo.

Ibada ya mazishi ya Kiplagat, ambaye alikuwa mwandani wa rais wa zamani marehemu Daniel arap Moi, ilifanywa katika eneo la Cheplambus, Kaunti ya Baringo.

Gavana wa Kaunti ya Turkana, Bw Josphat Nanok, alisema jamii nyingi za Bonde la Ufa tayari zimeonyesha wazi misimamo yao kuhusu BBI na uchaguzi wa urais 2022, kwa hivyo viongozi wote wanafaa kuzungumza kwa sauti moja.

Kufikia sasa, Bunge la Kaunti ya Baringo pekee ndilo limetupa nje Mswada wa BBI, kati ya mabunge 12 ambayo yameipigia kura.

“Tuna mwelekeo wa BBI na kura ya mwaka ujao. Ninachoomba ni watu wote wa Bonde la Ufa tuzungumze kwa sauti moja na tutoe uamuzi mmoja utakaosaidia Wakenya na watu wa Bonde la Ufa,” akasema Bw Nanok.

Wito sawa ulitolewa na Seneta wa Narok, Bw Ledama ole Kina, ambaye alisihi vigogo hao wawili kuwa hakuna haja yao kutofautiana. “Nyinyi ni sawa na watoto wa tumbo moja. Lazima muunganishe jamii ya Wakalenjin,” akasema.Hata hivyo, katika hotuba yake Dkt Ruto alisema yeye na Seneta Moi hawana uadui.

“Nataka kuwahakikishia kwamba tuko pamoja, sio kama Wakalenjin bali kama Wakenya ili kustawisha maendeleo,” akaeleza Naibu Rais.

Uhasama kati ya wawili hao ni jambo la wazi.Wakati mmoja Dkt Ruto alikatazwa kuingia katika boma la Mzee Moi alipokuwa akiugua.Alisafiri hadi mlangoni lakini akaambiwa asubiri, na baadaye akaelezwa hangemwona sababu alikuwa akipumzika.

Hivi majuzi, wawili hao walizozana kuhusu aliyestahili kupewa ‘baraka’ za wazee ili kuwa msemaji wa kisiasa wa jamii ya Kalenjin.Majuma kadha yaliyopita, Seneta Moi alielekea kukutana na wazee wa kijamii lakini msafara wake ulizuiwa na vijana waliokuwa wakiimba nyimbo za kumsifu Dkt Ruto.

Baadaye, alifanikiwa kupokea ‘baraka’ hizo ilhali pia Dkt Ruto alikuwa ameshazipokea.Wakati huo huo, Naibu Rais alitoa wito kwa vijana wajisajili katika taasisi za elimu ya kiufundi ili wapate ajira.

ikiwemo serikalini.Alisema wakati huu ambapo kuna miradi mingi ya maendeleo, kuna nafasi za ajira za kiufundi lakini vijana hawatazipata ikiwa hawana ujuzi unaostahili.

You can share this post!

Polisi kukamatwa kwa kutofika kortini

Mutua alia Kalonzo ameteka BBI Ukambani