• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Raia wa Nigeria afikishwa Kortini kwa wizi wa muda wa maongezi kwa kampuni ya jamii Telkom

Raia wa Nigeria afikishwa Kortini kwa wizi wa muda wa maongezi kwa kampuni ya jamii Telkom

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Nigeria aliyejaribu mara 53 kuiba muda wa maongezi kutoka kwa kampuni ya mawasiliano ya Jamii Telkom Jumatano aliachiliwa kwa dhamana huku polisi wakiendelea kumchunguza.

Hakimu mwandamizi Bi Carolyne Muthoni Njagi aliamuru mshukiwa huyo wa uhalifu wa kimitandao Bw Tokundo Abiondun Banjo awe akiripoti kwa afisa anayechunguza kesi hiyo Yvonne Anyango CFE hadi uchunguzi ukamilike.

Hakimu alifahamishwa Bw Banjo alikuwa ameandikisha laini 14 za simu zilizotumika katika majaribio ya kuiba muda wa maongezi ili wauze pesa tasilimu.Bi Njagi alimwamuru mshukiwa huyo alipe dhamana ya Sh100,000 pesa tasilimu.

Pia aliagizwa awasilishe wadhamini wawili raia wa Kenya watakaotia sahihi stakabadhi kuhakikisha mshukiwa huyo amefikishwa kortini.Mahakama ilimwagiza Bw Banjo awe akiripoti katika kituo cha polisi cha Muthaiga kaunti ya Nairobi kila siku.

Bi Njagi aliagiza mshukiwa huyo arudishwe mahakamani tena mnamo Agosti 12, 2021 kufunguliwa mashtaka ya kula njama kutenda uhalifu na wizi wa Sh100,000.Bi Njagi alisema uchunguzi wa uhalifu wa kimitandao wahitaji kupigwa darubini kali ili washirika wakuu watiwe nguvuni kwa lengo la kuusambaratisha.

“Mshukiwa huyu ni mmoja wa genge la wahalifu wa wizi wanaotumia mitandao kujipatia pesa kwa kuuza muda wa maongezi ya makampuni ya mawasiliano,”Bi Anyango alisema.Bi Anyango alieleza mahakama Banjo alifika katika afisi za Jamii Telkom kuripoti laini zake za simu zimefungwa.

Mahakama ilielezwa laini hizo 14 za mshukiwa huyo zilikuwa zinachunguzwa kwa vile zilitumika mara nyingi kujaribu kuiba muda wa maongezi.Mahakama ilielezwa mshukiwa huyo hana makazi maalum na akiachiliwa kwa dhamana atatoroka.

Lakini wakili anayemwakilisha raia huyo wa kigeni aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema “ameoa Mkenya na hawezi toroka familia.”Akitoa uamuzi Bi Njagi alisema uchunguzi utakaofanywa niwa kimitandao na haumshirikishi Bw Banjo.

Hakimu alisema laini za simu za mshukiwa huyu zimezimwa na polisi watazichunguza kwa usaidizi wa watalaam wa kiufundi wa kampuni za mawasiliano.

  • Tags

You can share this post!

Lynn anaamini ipo siku watakubali kazi yake katika uigizaji

Vikundi vya kutetea haki vyalalamika kuahirishwa kwa...