• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:50 AM
Raia waingiwa na hofu polisi wakiendelea kujiua

Raia waingiwa na hofu polisi wakiendelea kujiua

NA BENSON MATHEKA

WASIWASI umekumba Wakenya kuhusu usalama wao kutokana na ongezeko la visa vya maafisa wa polisi wanaopaswa kuwalinda kuua familia zao na kujiua kutokana na matatizo ya akili.

Hali hii inaendelea kusumbua Huduma ya Polisi (NPS) huku visa hivi vikiendelea kutokea licha ya kuwepo kwa mpango wa kuwapa maafisa wa polisi ushauri wa kisaikolojia.

Kinachozua wasiwasi ni kuwa maafisa wanaohusika ni wa umri mdogo na ambao ni tegemeo la kikosi hicho siku zijazo.

Katika kisa cha hivi punde, afisa wa polisi Antony Mwangi Njuguna, 29 alimuua mkewe Maureen Moraa Kiriago, 27 kwa kumpiga risasi kabla ya kujiua. Kisa hicho kilitokea katika mji wa Migori Jumapili.

Majirani walisema kwamba wawili hao waligombana kabla ya milio ya risasi kusikika ndani ya nyumba yao. Mnamo Januari mwaka huu, afisa wa polisi Dorcas Chebet alimpiga risasi mumewe Abed Ondari ambaye pia ni afisa wa polisi kabla ya kujilipua kwa risasi ndani ya nyumba yao katika kituo cha polisi cha Kiungani, Kaunti ya Trans Nzoia.

Kisa hiki kilifuatia kingine Desemba 2021 ambapo afisa wa polisi alimuua mkewe na watu wengine watano kwa kuwapiga risasi eneo la Kabete, Nairobi. Afisa huyo alijiua pia kwa kujipiga risasi.

Mwezi huo, afisa wa polisi alijitia kitanzi katika Kaunti ya Mombasa na kuacha ujumbe akisema alikuwa amezongwa na madeni.

Mapema mwaka 2021, Caroline Kagongo, afisa wa polisi aliyekuwa akihudumu Nakuru aliwaua watu wawili, mmoja akiwa afisa mwenzake wa polisi kabla ya kujiua akiwa nyumbani kwa wazazi wake.

Wanaharakati wanasema kuwa maafisa wanaosumbuliwa na mafadhaiko ni hatari kwa raia wanaopaswa kupewa ulinzi.

“Kwa mfano, chukua kisa ambacho afisa wa polisi aliwamiminia risasi raia watano wasio na hatia eneo la Kabete baada ya kumuua mkewe. Afisa wa polisi aliye na matatizo ya akili ni hatari kwa raia pia. Ikiwa wanaangamiza familia zao, je itakuwaje kwa raia?” anasema mwanaharakati Imran Ali.

Ingawa maafisa wakuu wa polisi na wizara ya Usalama wa Ndani wanasema kwamba wamechukua hatua za kukabiliana na hali hii, kuongezeka kwa visa vya maafisa kutekeleza mauaji hasa familia zao na kujiua, kama hali inayotishia usalama wa raia.

“Huduma ya polisi (NPS) imeanza mpango wa kuhamasisha maafisa wote kukabiliana na matatizo ya akili ili waweze kutimiza majukumu yao ya kutoa usalama na ulinzi nchini,” alisema Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai.

Mpango huo unalenga kuwawezesha maafisa wa polisi wa viwango vyote kukabili matatizo ya kiakili wanayopata kutokana na hali ya kazi yao.

Hata hivyo, Bw Ali anasema uchunguzi wa kina unafaa kufanywa ili kukabiliana kikamilifu na hali hii kabla ya kugeuka kuwa tishio kwa usalama wa raia.

“Maswali ambayo yanafaa kuwa msingi wa uchunguzi huo ni kama vile, kwa nini maafisa wanaohusika na visa hivi ni wale wa umri wa chini kuanzia miaka 24 hadi 32 na kwa nini wengi ni wale wa vyeo vya chini,” asema.

  • Tags

You can share this post!

STEVE ITELA: Wahifadhi mazingira wakataa marekebisho ya...

Gideon Moi asema ufisadi ndio chanzo kikuu cha umaskini

T L