• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Raila ataka serikali ilegeze masharti ya ibada

Raila ataka serikali ilegeze masharti ya ibada

Na CHARLES WASONNGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ameunga mkono pendekezo la baadhi ya viongozi wa kidini kwamba waruhusiwe kurejelea ibada zao kawaida wakiahidi kuendelea kuzingatia masharti ya kuzuia kuenea kwa corona.

Bw Odinga Alhamisi aliahidi kuwa atawasilisha ombi rasmi kwa serikali ili makanisa yapewe nafasi ya kuendesha ibada zao na shughuli nyinginezo.

“Nakubaliana nanyi kwamba wakati huu ambapo shule na taasisi zingine za kielimu zimeruhusiwa kurejelea masomo, makanisa pia yafunguliwe kikamilifu huku yakizingatia kanuni za Wizara ya Afya za kuzuia kuenea kwa Covid-19. Kwa hivyo, nitawasilisha ombi rasmi kwa serikali kuhusu suala hili,” Bw Odinga akasema alipokutana na baadhi ya viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu, Nairobi, kuwarai kuunga mkono mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa BBI.

Akiwasilisha ombi hilo kwa niaba ya viongozi hao wa kidini, Askofu Kepha Omae wa Kanisa la Redeemed Gospel Church, alisema makanisa yamejitolea kuzingatia masharti ya kuzuia kuenea kwa corona kwa manufaa ya waumini wao.

“Tunakuomba uingilie kati ili serikali iweze kuruhusu makanisa yetu kuendesha kurejelea taratibu za kawaida za ibada zetu ili kufanikisa wajibu wetu kama kanisa. Kama viongozi wa kidini, tuko tayari kuhakikisha kuwa kanuni zote za Wizara ya Afya za kuzuia kuenea kwa corona zinazingatiwa na waumini wetu,” akasema.

Mnamo Januari 25, Mwenyekiti wa Baraza la Kidini kuhusu Covid-19 Askofu Mkuu Anthony Muheria alilegeza masharti ya kudhibiti kuenea kwa Covid-19 katika maeneo ya ibada kwa kuruhusu sala za watoto (Sundaye School) na Madrassa.

Hata hivyo, Askofu Muheria aliagiza kuwa wasimamizi wa makanisa la misikiti sharti wahakikishe kuwa masharti ya Wizara ya Afya kama vile watoto kuvalia barakoa, kunawa kila mara na kukaa umbali wa mita moja, yanazingatiwa.

You can share this post!

Kane kusalia nje kwa muda mrefu baada ya kupata jeraha la...

Motisha tele kambini mwa Kenya Morans baada ya mwanavikapu...