• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Rais Ruto ‘aahirisha’ El Nino, akisema haitanyesha kama ilivyotabiriwa

Rais Ruto ‘aahirisha’ El Nino, akisema haitanyesha kama ilivyotabiriwa

NA LABAAN SHABAAN

RAIS William Ruto Jumapili, Oktoba 22, 2023, alisema kuwa nchi haitashuhudia mvua ya El Niño kama ilivyotabiriwa na Idara ya Hali ya Hewa Kenya (KMD).

Akizungumza katika ibada moja ya kanisa, eneo la Riruta, jijini Nairobi, Rais alisema kwamba idara ya hali ya anga ilisema badala ya El Niño,  kutakuwa na mvua kubwa.

“Hata juzi mliskia huenda kukawa na El Nino ambayo itaharibu mali. Lakini Mungu ni nani! Mmesikia wale watu (Idara ya Hali ya Hewa) wamesema hiyo El Nino haitakuwepo. Wamesema kutakuwa tu na mvua kubwa, lakini haitafika pale pa kuharibu. Si tunamshukuru Mungu jamani?” Rais aliwaambia washiriki kwenye kanisa hilo.

“Tumejipanga kwa hii mvua ambayo tutapata. Tumepanga wakulima watuzalishie chakula tena ili tuwe na mavuno mengine Januari ama Februari,” aliongeza huku akiushambulia Upinzani kwa maandamano uliofanya dhidi ya serikali.

Kadhalika, Dkt Ruto alisema Mungu alijibu maombi ya kitaifa yaliyofanyika Februari 2023, akisema alileta mvua nchini.

 

“Tulienda katika Uwanja wa Nyayo na tukamwomba Mungu. Wengine walituchekelea  wakisema, angalia hawa! Eti Rais mzima ameenda hapo Uwanja wa Nyayo kuomba? Mungu ametupatia mvua. Ametupatia mvua ambayo hatujapata kwa miaka minne,” kiongozi wa nchi alisema.

Rais aliahidi kuongeza rasilimali katika sekta ya kilimo ili kuimarisha mikakati ya kufikia utoshelevu wa chakula nchini.

Kwa mujibu wa ripoti ya Agosti 30, 2023 ya KMD, mvua isiyo ya kawaida itashuhudiwa kati ya miezi ya Oktoba–Novemba–Disemba.

Kaunti zimetenga angalau Sh15 bilioni kukabili na kudhibiti athari za mvua hizo.

Pia, Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema zaidi ya Sh10 bilioni zitatumiwa kudhibiti hali katika maeneo kame.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ugali Pambana: Wanachuo sasa wala ugali kwa harufu ya nyama...

Jinsi mwanamume aliyebakwa anaweza kulinda ushahidi

T L