• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Ugali Pambana: Wanachuo sasa wala ugali kwa harufu ya nyama kupambana na hali ngumu ya maisha

Ugali Pambana: Wanachuo sasa wala ugali kwa harufu ya nyama kupambana na hali ngumu ya maisha

NA LABAAN SHABAAN

MTAA wa KM, mkabala na Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), viungani mwa jiji la Nairobi, ni kituo cha wanafunzi cha biashara.

Nyakati za mlo, hasa mchana, wanafunzi husongamana mikahawani kwa chakula cha bei nafuu.

Hoteli hizi huwa na ushindani sana na hubidi wamiliki kuwa wabunifu kuvutia wateja, hasa nyakati hizi ambapo wananchi wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Hili limewasukuma kiasi cha kulemewa na bei ya nyama. Kwa hivyo, ‘ugali pambana’ huwa afueni kwao.

Ugali Pambana ni mlo unaojumuisha mifupa yenye nyama kidogo na supu na huandaliwa na sima.

Chakula hiki vile vile huitwa ‘ugali mlima’ huku wengine wakikiita ‘Ugali na meat on bones’ ama ‘pambana ng’ang’ana.’

Kwa miaka kumi, mapochopocho haya yamepanda bei kutoka Sh20 hadi Sh100.

“Mnamo 2013, chakula hiki kilikuwa Sh20!” Amakoye Brian alishangaa kuona jinsi gharama imebadilika.

“Wasichojua wanafunzi wa zamani ni kuwa kama huna Sh70 hapa KM, huwezi kupata kitu cha kula katika hoteli unayopenda,” alisema Ledama Kiruntare akilalamikia hali ngumu ya maisha.

Baadhi ya mikahawa inayouza Ugali Pambana kwa wanafunzi wa KU ni Blessed Café, Lakers Dishes, Mid City kutaja tu baadhi.

Taifa Leo ilizungumza na baadhi ya wanafunzi wanaokata kiu ya nyama kwa kula chakula hiki kinachopamba menu ya hoteli nyingi.

Kauli za baadhi yao zilisheheni utani, wengine wakisema ni sawa na kula sima kwa mifupa mikavu, au uvumi wa nyama na stori za nyama.

“Chakula hiki ni ugali, supu, mifupa na harufu ya nyama,” mwanafunzi mwengine, Eric Gitonga alisema.

“Ugali pambana ni mlo nilioupenda sana nilipokuwa chuoni,” Nicholas Muriiki alisifu.

Endapo wanafunzi hawa wangepiga abautani na kununua ugali kwa nyama, wangehitajika kulipa kuanzia angalau Sh150.

Wanafunzi wanasema hii ni njia ya kuokoa pesa na pia kutafuta mbinu ya kukata kiu ya nyama.

 

  • Tags

You can share this post!

Uhuru akataa mistari ya Gachagua

Rais Ruto ‘aahirisha’ El Nino, akisema haitanyesha kama...

T L