• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Saa za kafyu zaongezwa kaunti 13 zilizoko Magharibi, Nyanza

Saa za kafyu zaongezwa kaunti 13 zilizoko Magharibi, Nyanza

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imeongeza muda wa kafyu katika kaunti 13 zilizoko Magharibi mwa Kenya kama hatua ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Kuanzia Ijumaa, Juni 18, 2021, saa za kafyu sasa zitaanza saa moja jioni hadi saa kumi alfajiri badala ya saa nne za usiku hadi saa kumi alfajiri katika kaunti za Busia, Vihiga, Kisii, Nyamira, Kakamega, Kericho, Bomet, Bungoma, Trans Nzoia, Kisumu, Siaya, Homa Bay na Migori.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, Alhamisi alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kaunti hizo kwa ujumla kuandikisha kiwango vya maambukizi ya corona cha asilimia 21 ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa cha asilimia tisa.

Alitaja kaunti hizo, kila moja au kwa ujumla, kama maeneo yenye maambukizi ya juu ya corona, almaarufu “Covid-19 hotspot zone”.

“Amri ya kutotoka nje itadumishwa katika maeneo hayo kuanzia saa moja za jioni hadi saa kumi alfajiri,” akasema Bw Kagwe kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Hata hivyo, kafyu itaendelea kudumishwa maeneo mengine nchini kuanzia saa nne za usiku hadi saa kumi za alfajiri kila siku ilivyo sasa.

“Watu wanashauriwa kupunguza safari za kuingia na kuondoka katika maeneo hayo yenye maambukizi ya juu ya Covid-19,” Bw Kagwe akasisitiza.

Waziri huyo pia alisema masoko yote ya wazi na yale ya mifugo katika kaunti hizo 13 yamefungwa sawa na mikutano aina yoyote na mikutano ya maombi.

“Hafla zinazoandaliwa nyumbani na shughuli zozote za michezo pia zimesitishwa kwa muda usiojulikana. Mazishi ya aina yoyote pia sharti yafanywe baada ya saa 72 na ni watu 50 pekee wataruhusiwa kuhudhuria kila moja ya hafla kama hizo,” Bw Kagwe akaeleza.

“Ibada zote za kawaida makanisani, misikitini, hekaluni au maeneo mengine ya maabadi pia zimepigwa marufuku kwa kipindi cha siku 30,” akaongeza.

Bw Kagwe pia aliwashauri waajiri kuwaruhusu wafanyakazi wao wafanye kazi kutoka nyumbani isipokuwa wale ambao wanatekeleza majukumu muhimu.

“Ushauri huu ni kwa waajiri katika sekta za umma na zile za kibinafsi,” akafafanua.

Bw Kagwe pia alisema shughuli za harusi au hafla za kitamaduni katika kaunti hizo sasa zitahudhuriwa na watu wasiozidi 30 hadi wakati usiojulikana.

Masharti haya mapya yamtolewa na Waziri Kagwe siku moja baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kuonya kuwa huenda serikali ikaongeza masharti mengine ya kuzuia kuenea kwa corona katika kaunti za Nyanza na Magharibi mwa Kenya kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya ugonjwa huo hatari.

You can share this post!

SRC yazima nyongeza ya mishahara katika sekta ya umma

Ukraine yakomoa Macedonia Kaskazini na kusajili ushindi wa...