• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Serikali kugawana malipo na wauguzi wanaotumwa UK

Serikali kugawana malipo na wauguzi wanaotumwa UK

Na NASIBO KABALE

SERIKALI itapata asilimia fulani ya baadhi ya pesa watakazolipwa wauguzi wanaofanya kazi Uingereza kufuatia mkataba uliofanywa mwaka huu kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu Boris Johnson.

Mkataba huo ni tofauti na wa hapo awali ambapo wauguzi wangejisajilisha kivyao na kufanya kazi nchini Uingereza pasipo serikali kupata chochote kutokana na huduma zao.Aidha, mkataba huo ni sawa na uliofanywa kati ya Kenya na Cuba uliowezesha serikali kuwaleta nchini madaktari 100 kutoka Cuba waliolipwa kupitia serikali yao.

Serikali ya Cuba na madaktari wao hupata hela kutokana na mkataba huo.Bado haijabainishwa ni kiasi kipi cha hela kitakachogawiwa wauguzi na serkali kwa kila muuguzi atakayeajiriwa Uingereza.

Katibu wa Wizara ya Afya Susan Mochache amepangiwa kuongoza wajumbe wanaojumuisha maafisa wakuu katika Wizara ya Afya na Wizara ya Leba katika muda wa majuma machache yajayo kukamilisha masharti ya mkataba huo, duru zilieleza Taifa Jumapili.

Taifa Jumapili ilipowasiliana na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na Katibu wa Wizara Mochache kuhusu suala hilo, wote waliahidi kutoa taarifa baada ya majadiliano.

“Tungali tunamalizia mazungumzo ya kina,” alisema Kagwe.Kufikia sasa, wauguzi 3,329 wameashiria nia ya kujisajilisha kwa kazi hizo na watakaofuzu wanatarajiwa kusafiri Uingereza katikati mwa Oktoba.

Sawia na mkataba kati ya Cuba na madaktari waliotumiwa serikali ya Kenya, maelezo ya kina kuhusu jinsi wauguzi hao watakavyolipwa bado hayajawekwa wazi huku Ubalozi wa Uingereza ukitangaza tu kwamba wataalam wa afya ambao hawajapata kazi watasajiliwa kufanya kazi katika Huduma ya Kitaifa ya Afya Uingereza (NHS).

Wauguzi waliotuma maombi ya kazi na kusafiri Uingereza hapo awali vilevile watapata fursa ya kujisajili kupata uraia na kupokea asilimia 100 ya malipo yao.

Hata hivyo, kitengo hiki kitakuwa na mkondo maalum wa kufanyia kazi Uingereza ambapo asilimia fulani ya malipo waliyoafikiana ikienda kwa serikali.Aidha, watahitajika kufanya kazi katika sekta ya afya nchini Kenya baada ya muda fulani ulioafikiwa.

Wauguzi hao wanahitajika kuwa na shahada ya digrii katika taaluma ya uuguzi kutoka kwa taasisi inayotambuliwa, leseni kutoka kwa Baraza la Wauguzi, cheti halisi cha nidhamu kutoka kwa polisi na ithibati kwamba hawajawahi kuajiriwa na sekta ya umma au ya kibinafsi.

Ingawa haikujumuishwa katika tangazo la Wizara ya Leba na Masuala ya Jamii, wauguzi hao wanahitajika kuwa na tajriba ya angalau miezi 18.

Watahitajika pia kufanya majaribio maalum ya kupima ufahamu wao wa Kiingereza pamoja na ujuzi wa kompyuta kutoka kwa taasisi ya Uingereza kuhusu uuguzi na ukunga.

Watakaoshiriki jaribio la Kiingereza ni sharti wahitimu kiwango cha chini zaidi kwa jumla cha alama saba ingawa alama 6.5 katika uandishi itakubalika pamoja na kiwango cha saba katika uandishi, kusikia na kuzungumza.

Japo maelezo ya kina kati ya wahudumu wa afya, serikali ya Kenya na Uingereza hayakuwekwa bayana mara moja, ubalozi wa Uingereza ulisema kutakuwa na matokeo chanya kutokana na ushirikiano huo. kupitia usimamizi bora wa uhamiaji kama vile kiasi fulani cha pesa zinazotumwa nyumbanin na wahudumu wa afya.

You can share this post!

Mudavadi ataka BBI kuangaliwa upya

Raila tosha 2022, Joho asema