• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Serikali yatafuta Sh162 bilioni za matumizi miezi miwili tu baada ya kupitisha bajeti ya Sh3.74T

Serikali yatafuta Sh162 bilioni za matumizi miezi miwili tu baada ya kupitisha bajeti ya Sh3.74T

NA JULIANS AMBOKO

HUENDA serikali ikaendelea kuwatoza Wakenya ushuru zaidi ili kulipia mishahara na kufadhili bajeti ya ziada, baada yake kupendekeza kuchukua mikopo zaidi.

Takwimu mpya kutoka Hazina ya Kitaifa zinaonyesha kuwa serikali inapanga kuongeza bajeti ya mwaka huu kwa Sh162 bilioni, hatua itakayoifikisha bajeti ya mwaka huu hadi Sh3.91 trilioni.

Kiwango kikubwa cha nyongeza hiyo ya bajeti kitaelekezwa kwenye ulipaji wa mishahara na masuala mengine.
Serikali imepanga kuongeza bajeti ya ulipaji mishahara kutoka Sh2.54 trilioni zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge la Kitaifa mnamo Juni hadi Sh2.68 trilioni.

Fedha za kulipia mishahara zinaongezwa kwa asilimia 5.8 huku fedha za kufadhili miradi tofauti zikiongezwa kwa asilimia 1.6 pekee, hilo likiwakilisha Sh827 bilioni.

Hilo linamaanisha kuwa pengo la bajeti iliyosomwa Juni litaongezeka kutoka Sh761 bilioni hadi Sh864 bilioni. Mwelekeo huu unaashiria kuwa serikali imekosa kuzingatia ahadi ya kutotumia fedha nyingi katika masuala yasiyo muhimu kwa raia. Hii ni huku wananchi wakiendelea kuteseka kutokana na viwango vikubwa vya ushuru.

Hatua hiyo pia inamaanisha serikali italazimika kukopa Sh415.3 bilioni kutoka kwa taasisi tofauti za kifedha nchini, hilo likiwa kinyume na Sh316 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge.

“Pengo lililopo la Sh864 bilioni litafadhiliwa na mikopo ya Sh448.7 bilioni kutoka nje na mikopo ya Sh415.3 bilioni kutoka taasisi za kifedha humu nchini,” ikasema Wizara ya Fedha kwenye tathmini yake kuhusu hali ya fedha 2023.

Aina mpya za ushuru zilizopendekezwa na Sheria ya Fedha 2023 zilianza kutekelezwa Septemba 1. Zinajumuisha Ushuru wa Vifaa vya Kidijitali katika kiwango cha asilimia tatu ya mapato ya wale wanaoendesha shughuli tofauti za kifedha kupitia mitandao.

Ushuru mwingine ulioanza kutekelezwa ni ule wa bidhaa za mafuta (asilimia 16) na makato ya hazina ya nyumba, yanayojumuisha asilimia 1.5 ya mshahara anaolipwa mfanyakazi. Waajiri pia wanakatwa ushuru wa asilimia 1.5 kufadhili mpango huo.

Katika kile kinachoonyesha hatua ya serikali kutotosheka na ‘vita’ vyake vya ushuru dhidi ya Wakenya, imependekeza Ushuru Maalum wa Magari. Wakosoaji wamesema huenda hatua hiyo ikawaathiri pakubwa Wakenya, hasa wenye mapato ya kadri na wale wanaotegemea biashara ndogondogo.

Kinaya ni kuwa, serikali inapendekeza kuongeza kiwango cha bajeti mwaka huu, licha ya makusanyo ya fedha katika miezi ya Julai na Agosti kupungua kwa Sh58.7 bilioni, ikilinganishwa na kiwango kilichotarajiwa.

“Utekelezaji wa bajeti katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka wa kifedha wa 2023/24 umekuwa mzuri, ingawa tumekuwa tukiandamwa na changamoto katika ukusanyaji wa mapato,” ikasema Hazina ya Kitaifa.

Nyongeza mpya ya ushuru inakinzana na ahadi ya serikali kuchukua hatua kali kupunguza matumizi yake ya fedha katika masuala yasiyo muhimu.

  • Tags

You can share this post!

Kichuna Huddah Monroe asema Ruto atakuwa rais mbovu zaidi...

Wafanyakazi wa Delmonte wapata nyongeza ya mishahara...

T L