• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Serikali yatangaza vita na watengenezaji pombe haramu Mlima Kenya

Serikali yatangaza vita na watengenezaji pombe haramu Mlima Kenya

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kukabiliana na unywaji wa pombe na dawa za kulevya ili kuokoa kizazi kijacho, amesema katibu katika Wizara ya Usalama na Maswala ya Ndani Dkt Karanja Kibicho.

Amesema pombe haramu na bangi imeathiri vijana wengi nchini na serikali inafanya juhudi kupambana na wapikaji pombe haramu.

“Tangu tuanze kupambana na pombe haramu mwaka wa 2015, vijana wapatao 30,000 wameangamia na hata kufariki kutokana na pombe haramu. Kwa hivyo, serikali haitaketi kitako kuona vijana zaidi wakifa ovyo ovyo,” alisema Dkt Kibicho.

Alisema serikali imeanza kampeni kali ya kupambana na upikaji wa pombe na uuzaji wa dawa za kulevya.

Mpango huo utaendeshwa katika eneo lote la Mlima Kenya ambako unywaji wa pombe umeathiri vijana wengi.

Alisema kwa muda wa miaka sita tangu wazindue mpango wa kuangamiza pombe haramu wamemwaga pombe ya chang’aa na kangara kiasi cha lita trilioni moja.

“Kazi ambayo imefanywa na walinda usalama inastahili kupongezwa kwa vile wamepunguza kwa kiasi kikubwa upikaji wa pombe,” alifafanua katibu huyo.

Aliyasema hayo mjini Thika aliposhuhudia pombe haramu, dawa za kulevya, na mashine za kamari zikichomwa hadharani.

Mashine za kamari zikiteketezwa mjini Thika, Septemba 22, 2021. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliridhishwa na wakazi wa kijiji cha Makwa kilichoko Gatundu Kaskazini.

Hata alisema hata wake wa wanaume wa kijiji hicho wameanza kuwa wajawazito baada ya waume zao kuachana na ulevi wa kupundukia.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alipongeza juhudi za serikali ya kupambana na pombe haramu na dawa za kulevya.

“Iwapo serikali inataka kufaulu, ni sharti wawape polisi magari ya kutosha ya kuzunguka maeneo tofauti,” alisema Bw Wainaina.

Alisema hapo awali alitoa pikipiki nne za kusaidia polisi wanapopambana na pombe haramu.

Alisema mambo hayo yote ya kuangamiza pombe yanastahili ushirikiano kati ya wananchi na serikali ili yafanikiwe.

Aliitaka serikali kuingilia kati hali ya usalama ambao umezorota eneo la Thika Mashariki.

Alisema kwa muda wa miezi mitatu, watu wanne wameuawa kinyama katika kijiji cha Gatuanyaga, Thika Mashariki, jambo alilosema linastahili kuchunguzwa kwa makini.

Naye mtetezi wa haki za kibinadamu Bi Gladys Chania, alisema msako mkali unastahili kufanyiwa ili kuwanasa wahusika wa pombe haramu.

Alisema vijana wanastahili kuhamasishwa ili wasiendelee kujiingiza katika ulevi wa kiholela.

Kamishna wa Kaunti ya Kiambu Bw Wilson Wanyanga alisema wamenasa bangi na pombe haramu kwa wingi.

Alisema kwa muda mchache wamenaswa zaidi ya Lita 15,000 ya chang’aa, lita 430,000 za kangara, lita 4,800 za muratina, misokoto 9,723 ya bangi, na kilo zaidi ya 500 za bangi kwenye vifurushi.

Alisema sasa ndiyo wakati serikali imejitolea mhanga kukabiliana na janga hilo.

You can share this post!

QPR yaduwaza Everton kwenye Carabao Cup

Mabingwa watetezi Man-City wakomoa Wycombe na kutinga hatua...