• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Mbunge Alice Ng’ang’a alivyopendeza kwa kuvaa sare ya shule mpya ya Jamhuri iliyoko mjini Thika

Mbunge Alice Ng’ang’a alivyopendeza kwa kuvaa sare ya shule mpya ya Jamhuri iliyoko mjini Thika

NA LAWRENCE ONGARO

SHULE mpya ya upili ya Jamhuri Secondary School imezinduliwa kwa lengo la kusaidia wanafunzi wengi ambao hukosa kujiunga na kidato cha kwanza.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a ambaye aliongoza hafla ya uzinduzi huo, alisema ni hatua nzuri kwa sababu imewapunguzia wazazi mzigo wa kusafiri mbali kutafutia watoto wao shule.

Tayari wanafunzi wapatao 80 wamejisajili rasmi katika shule ya mseto ambayo iko katikati mwa mji wa Thika.

“Uzinduzi wa shule hii ni muhimu kwa sababu utapunguza mzigo ulioko katika shule nyingine za upili kama Broadway Secondary, Kimuchu Secondary, Queen of Rosary Secondary, na Thika Girls High,” alisema mbunge huyo.

Tayari mbunge huyo alitoa hundi ya basari ya Sh400,000 kuwa karo ya wanafunzi hao katika muhula huu wa kwanza.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a akiwa amevaa sare ya shule ya Jamhuri Secondary School. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Wazazi wa wanafunzi hao walishukuru hatua ya mbunge huyo kuzindua shule ya mseto kwa wana wao ambao wamejiunga na kidato cha kwanza.

“Mimi kama mbunge wenu ningetaka kuona ya kwamba kila mwanafunzi anahudhuria masomo bila kuchelewa. Pia nitahakikisha wanafunzi wanapata fedha za basari,” alifafanua mbunge huyo.

Alisema kampuni ya Safaricom imeahidi kutoa vitabu vya masomo kwa shule hiyo ya Jamhuri.

Alisema serikali iko tayari kuwatuma walimu waliohitimu ili kufunza katika shule hiyo.

Alisema tayari madawati 120 yalishafikishwa katika shule hiyo kusudi yatumiwe na wanafunzi hao.

Mkurugenzi wa elimu mjini Thika Bw Morris Sifuna alisema uzinduzi wa shule hiyo ulijiri wakati mwafaka.

Aidha msongamano utapungua katika shule nyingine katika mji wa Thika na vitongoji vyake.

“Nina imani kuwa walimu watakaoletwa hapa Jamhuri watakuwa wamehitimu na wanafunzi watapata mafunzo kamili,” alisema Bw Sifuna.

Alitoa wito kwa wazazi wasikae na wana wao nyumbani kwani shule hiyo ni ya mseto na karo pia ni nafuu kwa wazazi.

  • Tags

You can share this post!

Lopha Travellers yamulikwa abiria aliyerushwa nje basi...

Salaalaa! Mwanamume ashiriki kikao cha korti akiwa nusu uchi

T L