• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Shule ya Mwiki kupanuliwa

Shule ya Mwiki kupanuliwa

LAWRENCE ONGARO na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha ameahidi kuwa Shule ya Msingi ya Mwiki itafanyiwa ukarabati na kupanuliwa ili kuwapa wanafunzi mazingira mazuri ya masomo.

Aidha shule hiyo iliyoko Githurai itafanyiwa ukarabati sakafuni ili kuzuia matope mvua inaponyesha.

Waziri Magoha, alisikitishwa na idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hiyo.

Hata hivyo alisema ya kwamba serikali imepata eneo tofauti la ardhi ambako shule hiyo itapanuliwa zaidi ili wanafunzi wapate nafasi ya kusoma.

Alitoa hakikisho kuwa tayari shule hiyo imepata madawati 140 ambazo zitasaidia wanafunzi hao, hata ingawa idadi yao iko juu.

“Kuna madarasa mawili yanayostahili kurekebishwa mara moja na nina hakika serikali ina fedha za kutosha kukamilisha mradi huo,” alisema Prof Magoha.

Alitangaza ya kwamba mtihani wa kitaifa wa watahiniwa wa Darasa la Nane utaanza Machi 19, huku akiwataka wanafunzi kutokuwa na hofu kuhusu mtihani huo.

“Tunaelewa vyema wanafunzi walikuwa nyumbani kwa zaidi ya miezi tisa, na kwa hivyo tunajua jinsi ya kutunga mitihani yao. Kwa hivyo wanafunzi wasiwe na hofu kuhusu mitihani hiyo,” alisema waziri hiyo.

Alisema madawati tayari yamesambazwa kikamilifu katika maeneo tofauti.

Alitaja baadhi ya maeneo ambayo yamepokea madawati kwa asilimia 100 ni Kiambu, Nyeri, Nyahururu, na Murang’a.

Alisema wasichana wote walio wajawazito wataruhusiwa kufanya mitihani yao bila kutatizwa na yeyote.

“Kila mwanafunzi aliye na mimba ataruhusiwa kufanya mtihani katika mazingira tulivu,” alifafanua.

Wakati huo pia waziri alipeana barakoa kwa shule nzima ili wanafunzi wanufaike.

Waziri pia aliandamana na katibu katika wizara Belio Kipsang’ na washika dau wengine wa elimu.

Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alipongeza juhudi za waziri kutembelea shule hiyo ambayo idadi ya wanafunzi imefika 4,000.

Alisema tayari afisi yake kwa kushirikiana na serikali imepata kipande cha ardhi ekari tisa ambako kutajengwa madarasa mengine ili kupunguza msongamano ulioko katika shule ya msingi ya Mwiki.

“Idadi kubwa ya wanafunzi inasababisha hata walimu wenyewe wawe na ugumu kuwafunza wanafunzi hao. Kwa hivyo tukipata nafasi ya kuwasambaza kwingineko itakuwa ni sawa,” alisema Bw King’ara.

Kwa mfano, alisema, darasa moja kama Gredi ya Nne, kuna wanafunzi wapatao 250.

Alisema mji wa Ruiru unazidi kupanuka na kwa hivyo inahitaji mikakati tofauti kukidhi jinsi mambo yalivyo.

Shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 4, 000, na imekuwa vigumu kuafikia kikamilifu sheria na mikakati kusaidia kuzuia kuenea kwa Covid-19.

Kwenye ziara yake Jumatatu katika shule hiyo, hata ingawa waziri Magoha hakueleza wakati ambapo shughuli za upanuzi zitaanza, alisema serikali itahakikisha madarasa zaidi yamejengwa.

Prof Magoha pia aliahidi Mwiki Primary kupata uga, raslimali muhimu ambayo imeendelea kukosa katika shule hiyo.

“Ninaamini serikali ina pesa, na zitakapopatikana itapanuliwa,” akasema.

Wakati huo huo, Waziri alihimiza viongozi wa kisiasa waliochaguliwa eneo hilo kutumia mamlaka yao kushinikiza serikali kuiongezea shule hiyo ardhi.

Katika ziara hiyo kukagua shughuli za masomo zinavyoendelea, Prof Magoha alikuwa ameandamana na mbunge wa Ruiru, Bw Simon King’ara na seneta maalum, Bw Isaac Mwaura (ingawa Mwaura alibanduliwa wadhifa wake Jumatatu na chama tawala cha Jubilee kwa kukaidi sheria za chama).

“Viongozi wa kisiasa waliochaguliwa eneo hili, ninawahimiza mtumie mamlaka yenu kushinikiza serikali iongezee shule hii ardhi kwa minajili ya kuipanua ili watoto wetu wawe na mazingira bora ya masomo,” akawarai.

Seneta Mwaura amekuwa akiihimiza serikali kujenga madarasa zaidi katika shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi nchini, hasa baada ya kufanya ziara katika shule ya Mwiki Januari 2021 na kushuhudia mahangaiko ya wanafunzi.

You can share this post!

Sonko augua akiwa rumande, alazwa hospitalini

Ingwe yapata kocha wa 12 wa kigeni ndani ya miaka 12,...