• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Ingwe yapata kocha wa 12 wa kigeni ndani ya miaka 12, Mbelgiji Aussems anaanza kazi leo

Ingwe yapata kocha wa 12 wa kigeni ndani ya miaka 12, Mbelgiji Aussems anaanza kazi leo

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya, AFC Leopards wametambulisha Patrick Aussems kama kocha wao mpya Jumanne.

Aussems, ambaye majukumu yake ya kwanza yatakuwa kuongoza Ingwe katika raundi ya 64-bora ya Kombe la Betway Cup hapo Februari 13, anajiunga nayo baada ya kuongoza miamba wa Tanzania, Simba SC kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu 2018-2019. Alifikisha Simba katika robo-fainali ya Klabu Bingwa Afrika ilipoondolewa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-1.

Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 55, ambaye anatwaa mikoba ya ukufunzi kutoka kwa Mkenya Anthony ‘Modo’ Kimani, ana ujuzi wa miaka nyingi katika soka.

Beki huyo wa zamani wa klabu ya Standard Liege pia amenoa klabu nchini Ufaransa (ikiwemo katika kisiwa cha Reunion katika Bahari Hindi), Cameroon, Uchina, Congo Brazzaville na Uhispania na timu ya taifa ya Nepal katika kipindi cha miaka 30.

Aliwahi pia kuwa mkurugenzi wa kiufundi wa Benin pamoja na kuongoza klabu ya Al-Hilal kutoka Sudan. “Amehitimu na leseni ya ukocha ya Shirikisho la Soka Bara Ulaya (UEFA) PRO,” AFC Leopards ilitangaza kupitia mitandao yake ya kijamii Februari 9.

Aussems anatarajiwa kuwa na kipindi cha kwanza cha mazoezi na wachezaji Jumanne. Mbelgiji huyu ni kocha wa 12 wa kigeni wa Leopards tangu mwaka 2012 baada ya Jan Koops (Uholanzi), Luc Eymael (Ubelgiji), Zdravko Logarusic (Croatia), Ivan Minnaert (Ubelgiji), Stewart Hall (Uingereza), Dorian Marin (Romania), Rodolfo Zapata (Argentina), Nikola Kavazovic (Croatia), Marko Vasiljevic (Croatia), Andre Casa Mbungo (Rwanda) na Thomas Trucha (Czech).

You can share this post!

Shule ya Mwiki kupanuliwa

Ingwe yapata mpinzani mpya Betway Cup timu ya Taita Taveta...