• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Sonko atishia ‘kuanika Joho’

Sonko atishia ‘kuanika Joho’

NA MWANDISHI WETU

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, ametishia kufichua siri anazodai kufahamu kuhusu utawala wa Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho.

Mwanasiasa huyo wa Chama cha Wiper ambaye anajiandaa kuzindua kampeni zake za kushindania ugavana Mombasa alidai kuwa viongozi wa ODM Mombasa wameingia kiwewe kwa vile wanajua yale anayoweza kuyafanya katika kaunti hiyo.

“Ninajua udhaifu wao na ninaweza kuanika yale ninayoyajua kuwahusu hadi nishinde kiti hiki,” akasema.

Tangu Wiper inayoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais, Bw Kalonzo Musyoka, kumpa tikiti ya kuwania ugavana Mombasa, Bw Sonko amekashifiwa vikali na wapinzani wake wanaosema kaunti hiyo haihitaji kusimamiwa na gavana ambaye aling’olewa mamlakani kwingine.

Bw Sonko alitimuliwa uongozini Nairobi baada ya bunge la kaunti hiyo kumpata na makosa ya usimamizi mbaya, na juhudi zake kubatilisha uamuzi huo mahakamani ziligonga mwamba.

Viongozi wa ODM Mombasa wakiongozwa na Gavana Hassan Joho, wamekuwa wakipinga uamuzi wa Wiper kumpa tikiti ya ugombeaji.

Chama hicho kimemsimamisha Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, kumrithi Bw Joho atakayekamilisha kipindi chake cha pili uongozini Agosti.

Nassir alikabidhiwa tikiti ya ODM baada ya mashauriano na aliyekuwa mpinzani wake, mfanyabiashara Suleiman Shahbal, ambaye ameahidi kumuunga mkono na kukataa shinikizo kuwa mgombea huru.

Viongozi wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika kaunti hiyo pia walipinga ujio wa Bw Sonko.

Wakiongozwa na aliyekuwa seneta, Bw Hassan Omar, ambaye ndiye amepangiwa kuwania ugavana kupitia chama hicho, walisema Mombasa haihitaji viongozi waliotimuliwa kwa misingi ya kukosa maadili.

“Kujitosa kwangu katika kinyang’anyiro cha uongozi Mombasa ni kwa nia ya kuleta suluhisho kwa matatizo ambayo Gavana Hassan Joho alishindwa kusuluhisha katika hatamu yake,” akasema Bw Sonko.

Bw Nassir alisema yuko tayari kukabiliana na mpinzani yeyote uchaguzini akiwemo Bw Sonko.

Bw Musyoka alimshawishi Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, kuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko.

Awali, Bw Mbogo alikuwa amepanga kuwania ugavana na alikuwa tayari ashapewa tikiti ya muda.

  • Tags

You can share this post!

Jezi ya ‘Hand of God’ ya Maradona yazoa Sh1.1...

GWIJI WA WIKI: John Muli

T L