• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Jezi ya ‘Hand of God’ ya Maradona yazoa Sh1.1 bilioni mnadani

Jezi ya ‘Hand of God’ ya Maradona yazoa Sh1.1 bilioni mnadani

Na MASHIRIKA

JEZI iliyovaliwa na aliyekuwa mwanasoka nguli wa Argentina, Diego Maradona alipofunga bao kwa mkono almaarufu ‘Hand of God goal’ dhidi ya Uingereza katika Kombe la Dunia mnamo 1986 imezoa Sh1.1 bilioni mnadani.

Hicho ndicho kiasi kikubwa zaidi cha fedha kuwahi kupatikana kutokana na mauzo ya jezi ya mchezo wowote duniani.

Jezi hiyo ya samawati iliyokuwa ikivaliwa na Argentina ugenini, ilikuwa ikimilikiwa na mwanasoka wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Steve Hodge. Aliitia mnadani miaka 36 baada ya kubadilishana na Maradona mwishoni mwa mechi ya robo-fainali ya Kombe la Dunia katika uwanja wa Azteca nchini Mexico.

Argentina ilishinda mechi hiyo 2-1 huku bao lililofungwa na Maradona kwa mkono likimwacha hoi kipa Peter Shilton wa Uingereza.

Baada ya Maradona kuaga dunia mnamo Novemba 2020, Hodge aliwahi kusema kwamba jezi iliyovaliwa na nguli huyo wa Argentina haikuwa ya kuuzwa.

Lakini jezi hiyo iliyonadiwa katika jumba la Sotheby ilizoa kiasi kikubwa cha pesa kuliko Sh624 milioni au Sh936 milioni zilizotarajiwa awali. Jezi inayoshikilia rekodi ya kuzoa fedha nyingi zaidi duniani baada ya kutiwa mnadani ni ile iliyovaliwa na nguli wa mchezo wa baseball katika kikosi cha New York Yankees nchini Amerika, Babe Ruth. Jezi hiyo iliuzwa kwa Sh686.4 milioni mnamo 2019.

Hodge, 59, aliwakilisha timu ya taifa ya Uingereza katika makala mawili ya fainali za Kombe la Dunia na akachezea kikosi hicho mara 24. Aliwapa wasimamizi wa Makavazi ya Kitaifa ya Soka nchini Uingereza jezi hiyo ya Maradona kwa mkopo baadaye na imekuwa katika hifadhi hiyo kwa zaidi ya miaka 20.

Maradona anachukuliwa kuwa miongoni mwa wanasoka bora zaidi wa enzi zake duniani huku akichangia pakubwa ushindi wa Kombe la Dunia uliovunwa na Argentina nchini Mexico mnamo 1986 baada ya kupepeta West Germany 3-2 katika fainali.

Katika uhai na kipindi chake cha usogora, aliwahi pia kuvalia jezi za Boca Juniors, Barcelona, Sevilla na Newell’s Old Boys. Hata hivyo, umaarufu ulianza kumwandama akichezea Napoli ya Italia kati ya 1984 na 1991. Ni wakati huo alipovunja rekodi nyingi za dunia na kuweka jina lake katika mabuku ya historia kwa kuwa mwanasoka bora duniani wa kizazi chake.

Akiwa nahodha wa Napoli, aliongoza kikosi hicho kutwaa taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa mara ya kwanza mnamo 1986-87. Alisaidia waajiri wake hao kunyanyua taji la pili la Serie A mnamo 1989-90 na pia kuzoa mataji ya Uefa Cup, Coppa Italia na Italian Super Cup.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Real Madrid yang’oa Man-City na kufuzu kuvaana na...

Sonko atishia ‘kuanika Joho’

T L