• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Sonko kuwasilisha hati kwa IEBC kuidhinishwa kuwania ugavana

Sonko kuwasilisha hati kwa IEBC kuidhinishwa kuwania ugavana

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Sonko na mwaniaji Useneta Kiambu kwa tikiti ya UDA Karungo Thangw’a wanaweza kuwasilisha karatasi kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Hatua hii inafuatia kuondolewa kwa maagizo ya majaji John Mativo na Antony Mrima ya kuizima IEBC kupokea katarasi za uteuzi za Sonko na Thangw’a.

Lakini majaji David Majanja, Enock Mwita na Murungi Thande walisema wako na mamlaka ya kufutilia mbali maagizo hayo.

“Kila mlalamishi yuko huru kupewa fursa ya kuwasilisha kesi yake na maagizo kutolewa. Maagizo ya majaji hawa yalitolewa kabla pande zote kusikilizwa,” walisema majaji hao.

Mahakama ilisema Sonko na Thangw’a wanaweza kupeana karatasi lakini IEBC ina uwezo wa kutoa uamuzi ikiwa wawili hao watakubaliwa au la.

Na wakati huo huo Jaji Jairus Ngaah aliamuru kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kupinga uamuzi asiwanie Ugavana isikilizwe na Mahakama Kuu Mombasa.

Bw Sonko aliwasilisha kesi hiyo mahakama kuu ya Nairobi akipinga uamuzi wa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati kumnyima fursa ya kuwania Ugavana Mombasa.

Bw Chebukati alisema Sonko alitimuliwa Ugavana na Bunge la Seneti lililompata na hatia ya kushiriki ufisadi na utovu wa maadili.

“Kwa vile Sonko anawania Ugavana Mombasa, hii kesi inafaa isikilizwe na kuamuliwa kule. Naamuru kesi hii itajwe mbele ya Jaji anayesimamia Mahakama kuu Mombasa kwa maagizo zaidi,” aliamuru Jaji Ngaah.

Katika kesi hizo tisa Majaji David Majanja, Enock Chacha Mwita na Murungi Thande waliagiza ziunganishwe kwa vila zinahoji masuala sawa.

Majaji Enock Mwita (kushoto) David Majanja na Murungi Thande. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Majaji hao waliwaagiza wahusika wote wawasilishe mihutasari ya kesi hizo kufikia leo ( Juni 7).

Majaji hao walisema kesi hizo zitasikilizwa kwa pamoja na uamuzi mmoja tu kutolewa.

Kesi hizo zilishtakiwa katika Mahakama za Mombasa, Eldoret na Nairobi.

Jaji Koome aliagizwa zisikilizwe Nairobi na majaji hao watatu.

Mawakili John Khaminwa, Wilfred Nyamu, Assa Nyakundi , Jared Magollo na Titus Kirui wanaomwakilisha Sonko waliomba wapewe muda wa kutosha kutathmini kwa undani masuala nyeti ya sheria yanayozua utata yaamuliwe na kutoa mwelekeo ikiwa mmoja akishtakiwa kwa ufisadi anafaa kuwania kiti cha uongozi au la.

Majaji hao walielezwa na mawakili kwamba kipengee cha katiba nambari 6 kinastahili kufafanuliwa kabisa.

Mawakili wa Mike Sonko wakiwa kortini kuomba aruhusiwe kuwania Ugavana. PICHA | RICHARD MUNGUTI
  • Tags

You can share this post!

Messi aweka rekodi ya ufungaji mabao kimataifa

Wanne kati ya 58 wapitishwa kuwania urais

T L