• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Messi aweka rekodi ya ufungaji mabao kimataifa

Messi aweka rekodi ya ufungaji mabao kimataifa

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alipachika wavuni mabao yote matano katika ushindi mnono wa 5-0 uliosajiliwa na Argentina dhidi ya Estonia katika pambano la kirafiki lililochezewa Pamplona, Uhispania.

Argentina walishuka dimbani siku tatu baada ya kupepeta mabingwa wa Euro, Italia, 3-0 na kunyanyua taji la Finalissima ugani Wembley, Uingereza. Mabingwa hao mara mbili wa dunia (1986, 1978) sasa hawajapoteza mechi yoyote kati ya 33 zilizopita tangu Juni 2019. Walinyanyua taji la Copa America kwa mara ya kwanza tangu 1993 mnamo Julai 2021 na wakafuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar bila kushindwa.

Messi, 34, alifungia PSG mabao 11 pekee katika msimu huu wa 2021-22, idadi hiyo ikiwa yake ya chini zaidi katika kipindi cha miaka 16 iliyopita. Hata hivyo, amefufua makali yake kambini mwa Argentina huku ushirikiano mkubwa kati yake na wavamizi Lautaro Martinez na Angel Di Maria ukiwa mwiba mchungu kwa wapinzani.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Messi kufungia Argentina mabao matano katika mechi moja. Hadi kufikia Jumamosi, alikuwa amefaulu kufanya hivyo mara moja pekee kitaaluma – katika ushindi wa 7-1 uliovunwa na waajiri wake wa zamani, Barcelona, dhidi ya Bayer Leverkusen katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2012.

Bao la tatu lililofungwa na Messi dhidi ya Estonia lilikuwa lake la 84 kimataifa na lilimfanya kumfikia Ferenc Puskas aliyekuwa akishikilia nafasi ya nne kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika historia ya soka ya wanaume kimataifa.

Messi alipopachika wavuni bao lake la nne, alimpiku kigogo huyo wa zamani wa Hungary na sasa anasoma migongo ya Mokhtar Dahari wa Malaysia (89), Ali Daei wa Iran (109) na Ronaldo (117). Nyota huyu anatarajiwa kutua Qatar mnamo Novemba mwaka huu kutumia fursa yake ya mwisho kushinda Kombe la Dunia – taji la pekee ambalo hajawahi kunyanyua katika taaluma yake ya usogora.

Messi anajivunia jumla ya mabao 768. Amefungia Argentina (85), Barcelona (672) na Paris Saint-Germain (11). Ronaldo, 37, alifungia Man-United mabao 24 katika mashindano yote ya msimu wa 2021-22, na sasa anajivunia jumla ya magoli 815 kitaaluma.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Josef Bican wa Jamhuri ya Czech aliwahi kufunga mabao 805. Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Czech linadai kuwa mabao ya Bican aliyeaga dunia mnamo 2001 ni 821 huku shirika la kuhifadhi takwimu za wachezaji la The Rec.Sport.Soccer Statistics Foundation (RSSSF) likinakili mabao ya Bican kuwa zaidi ya 950.

Kinyume na FIFA inayoweka Cristiano Ronaldo wa Manchester United na Ureno kileleni mwa wafungaji bora kimataifa, RSSSF inashikilia kwamba Mjerumani Erwin Helmchen aliwahi kufunga mabao zaidi ya mabao 980 huku Mwingereza Ronald Rooke akicheka na nyavu za wapinzani zaidi ya mara 920.

Wanasoka nguli wa Brazil, Pele na Romario, pamoja na Puskas wa Hungary waliwahi pia kupachika wavuni zaidi ya mabao 700 japo idadi kamili ya kila mmoja haijabainishwa.

ORODHA YA FIFA YA WAFUNGAJI BORA DUNIANI:

Cristiano Ronaldo (2001 hadi sasa) – mabao 815

Josef Bican (1931-1955) – mabao 805

Romario (1979-2009) – mabao 772

Lionel Messi (2003 hadi sasa) – mabao 768

Pele (1957-1977) – mabao 757

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mbappe ndiye mwanasoka mwenye thamani kubwa zaidi duniani

Sonko kuwasilisha hati kwa IEBC kuidhinishwa kuwania ugavana

T L