• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Spika Wetang’ula almaarufu Papa wa Roma ataka ‘boychild’ kuwezeshwa

Spika Wetang’ula almaarufu Papa wa Roma ataka ‘boychild’ kuwezeshwa

NA BENSON MATHEKA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amesisitiza umuhimu wa elimu-jumuishi, hasa kuangazia elimu ya mtoto wa kiume.

Akihutubia washikadau wa elimu mnamo Jumamosi katika Shule ya Msingi ya Bungoma D.E.B katika eneo bunge la Kanduyi, Spika Wetang’ula alielezea wasiwasi wake kuhusiana na kutelekezwa kwa mtoto mvulana katika elimu.

“Hata katika kanisa langu, Kanisa Katoliki, niliona kwamba kati ya watoto 30 wanaoshiriki, 25 ni wasichana. Ni muhimu kuhakikisha kwamba mtoto mvulana anapata uangalizi unaostahili,” akasema spika Wetang’ula.

Spika aliwapongeza walimu kwa kujitolea kazini na wanafunzi kwa bidii yao.

Spika Wetang’ula aliongoza siku hiyo ya maombi katika shule hiyo, ambayo yalilenga kuwatia moyo wanafunzi wa Darasa la Nane wanapojiandaa kwa mtihani wa kitaifa wa KCSE, na wa mwisho chini ya mfumo wa elimu wa 8-4-4 nchini Kenya.

Alitoa shukrani zake kwa wazazi kwa usaidizi wao usioyumba, ambao umesaidia kuifanya Shule ya Msingi ya Bungoma D.E.B kuwa shule ya msingi ya pili kwa idadi kubwa ya watu nchini.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw Tobias Khisa, alifichua kuwa shule hiyo iliyoanza na wanafunzi 150 mwaka 1953, imeshuhudia idadi ya wanafunzi wake ikiongezeka hadi kufikia wanafunzi 4,800.

Alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanafunzi na walimu kuboresha upatikanaji wa elimu.

Dkt Wetang’ula pia alithibitisha anaunga mkono kufufuliwa kwa Kampuni ya Sukari ya Nzoia, akibainisha kuwa maendeleo makubwa yamepatikana katika kulipa madeni ya kampuni hiyo na kueleza matumaini yake kuhusu kufufua uchumi wa eneo hilo punde mgao wa bajeti ya ziada utakapopatikana.

Spika alihimiza nchi kuchangamkia mvua inayotarajiwa kunyesha, huku akiwataka wananchi kupanda mazao ya muda mfupi na serikali kuwekeza katika kukusanya maji.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na watu kadhaa mashuhuri, akiwemo Mbunge wa eneo hilo John Makali na mwenzake Majimbo Kalasinga (Kabuchai) na viongozi mbalimbali na madiwani.

  • Tags

You can share this post!

EPRA yapandisha bei ya petroli kutoka 211.64 hadi Sh217.36...

STAA: MVP Akinyi aliyeshindia Nyamira ubingwa wa hoki

T L