• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
STAA WA SPOTI: Huyu Fasila moto otea mbali kambini mwa Ulinzi Starlets

STAA WA SPOTI: Huyu Fasila moto otea mbali kambini mwa Ulinzi Starlets

NA AREGE RUTH

KATIKA kipindi kifupi cha uhamisho wa wachezaji kwenye Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL) mwezi Machi, wanajeshi wa Ulinzi Starlets walifanya sajili tatu za nguvu.

Hao ni kiungo Lavenda Akinyi kutoka Wadadia Women, mlinda-lango Judith Osimbo (Kibera Girls Soccer) na mshambuliaji matata Fasila Adhiambo (Kangemi Ladies).

Adhiambo, almaarufu Kamama, alikuwa kinywani mwa mashabiki msimu jana alipofunga mabao 15; mawili nyuma ya straika wa zamani wa Vihiga Queens, Topister Situma, ambaye alijiunga na Simba Queens katika Ligi Kuu ya Tanzania.

Kinaya ni kwamba alikuwa akitesa mabeki huku timu yake ya Kangemi Ladies ikiburuta mkiani ligini.

Lakini waliponea kushushwa daraja baada ya msimu kufutiliwa mbali.

Binti huyu alikuwa aking’aa uwanjani na darasani pia, kwani alifanya mtihani wake wa kidato cha nne katika shule ya upili ya mseto ya Dagoretti, Nairobi, mwaka jana.

Baada ya kumaliza masomo Desemba mwaka jana, timu nyingi ikiwemo Zetech Sparks na Ulinzi Starlets zilimmezea mate.

“Nitajiunga na chuo kikuu baadaye ila kwa sasa natafuta riziki,” Adhiambo, 19, aliambia Dimba.

Pia, alikuwa katika timu ya Dagoretti iliyowakilisha Kenya katika mashindano ya shule za upili Afrika Mashariki nchini Tanzania mwaka jana.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Ulinzi majuzi Februari kwa kandarasi ya muda usiojulikana.

Alidokeza kuwa wazazi wake walichangia pakubwa yeye kujiunga na wanajeshi.

“Ni ndoto ya wachezaji wengi kuchezea Ulinzi ikizingatiwa kwamba hapa kuna pia nafasi za kazi katika jeshi la taifa. Kando na kuwa nilitamani kuchezea timu hii,” anahoji.

Ilimchukua muda kumakinikia mfumo wa kocha.

Katika mechi yake ya kwanza ya ligi msimu huu, alichangia bao katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Kayole Starlets, uga wa Ulinzi Sports Complex, Nairobi. Amefunga magoli mawili katika mechi nne za KWPL. Ulinzi wako namba tatu na alama 29; tano nyuma ya vinara Gaspo Women.

Katika Kombe la Shirikisho la Soka (FKF Cup), ambalo Ulinzi wako robo-fainali, Adhiambo ndiye mfungaji bora na mabao sita.

Alivaa jezi ya timu ya taifa Rising Starlets mwaka 2019.

Alikuwa katika kikosi cha wasiozidi miaka 17 mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Kenya ilimaliza namba tatu huku akifunga magoli manane.

  • Tags

You can share this post!

Old Mutual wapiga jeki juhudi za Faith Mwende kukwea Mlima...

Mvua kubwa yatatiza Eid al-Fitr Mombasa

T L