• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Teuzi zote zifanywe kwa kuzingatia katiba bila ubaguzi

Teuzi zote zifanywe kwa kuzingatia katiba bila ubaguzi

Na KINYUA BIN KING’ORI

Kipengele cha 166 ibara ya 1 (b) cha katiba ya taifa hili linaloongozwa na Rais Uhuru Kenyatta kinaelezea wazi kuwa, Rais atateua majaji wengine wote, kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume ya huduma za mahakama (JSC).

Kabla sijaendelea na mada kuu ya leo, hebu nikukumbushe msomaji wangu mojawapo ya mamlaka ya Rais katika katiba mpya ya 2010 kifungu cha 131 ibara ya 2 (a) kinachosisitiza Rais ataiheshimu, kuifuata na kuilinda katiba.

Na ndivyo rais uhuru Kenyatta ameapa kuilinda na kuizingatia kwa kuiheshimu na kutenda vinginevyo itakuwa ni ukaidi, dharau, kutoiheshimu na kutoilinda katiba Kwa mujibu wa kiapo alichoapa alipoapishwa kuwa Rais wa jamhuri ya Kenya. Nikirejelea mada yangu, rais uhuru Kenyatta juma lililopita aliteua majaji 34 kati ya 40 waliokuwa wameteuliwa na Tume ya huduma za mahakama (JSC).

zaidi ya miaka miwili iliyopita, majaji hao tayari washaapishwa huku wengine 6 wakikosa kuteuliwa kwa visingizio visivyo na mbele wala nyuma. Nasema hivyo kwa sababu Rais amekosa kuelezea wakenya sababu za kuridhisha kwa nini amekataa katakata kuwateua majaji Weldon Korir, Profesha Joel Ngugi, George Odunga, Judith Omanga Cheruiyot, Aggrey Muchelule na Makori Evans Kiago licha ya kuwa kuidhinishwa na tume ya JSC.

Kwa kipindi kirefu sasa, rais uhuru Kenyatta amekuwa kiongozi anayekaidi maagizo mbalimbali ya korti sawia kuvunja vipengele vingi vya katiba ambayo ndiye Rais wa kwanza kutawala chini ya katiba hii mpya. Rais ni kiongozi aliyekula kiapo cha uaminifu kwa katiba hii kwa mujibu wa kifungu cha 262(13) na kwa namna yoyote anafaa kuwa mstari wa mbele kuifuata bila kulazimishwa na kufanya mambo kwa upendeleo au ubaguzi itakuwa sawa na kushangilia katiba ivunjwe na kila mtu.

Haiwi mfano bora kwa kiongozi wa taifa kuonyesha hadharani anakiuka katiba anapotekeleza majukumu yake, maana itaeleweka anayo nia mbaya kuinyonga katiba, katika jaribio ya kulazimisha maamuzi yake katika idara ya mahakama kwa kuteua majaji anaowataka yeye na kuwabagua wenye misimamo mikali kutetea katiba ni sawa na kuinyonga.

Hivyo, ajue kuteua majaji kwa upendeleo haitomsaidia kitu, hata kutumia hotuba zake kushambulia idara ya mahakama kutokana na maamuzi yake hasa uamuzi wa majuzi wa mahakama kuu kubatilisha BBI. Busara kwa Rais sasa ni kuteua majaji hao 6, anapaswa kumeza ukweli mchungu kwamba hana mamlaka yoyote kuchagua baadhi ya majaji katika orodha ya JSC, bali kuwateua wote bila kuchuja wala kupendelea, hivyo ndivyo kifungu cha 166 kinavyosema.

Je, huenda Rais anatumia majaji hawa 6 kuadhibu wao kutokana na maamuzi yao kortini? Je, labda huu ndio wakati Rais amepata nafasi ya kulipiza kisasi Kwa idara ya mahakama? Je, majaji kina prof Ngugi labda wanadhulumiwa kwa vile walikuwa miongoni mwao majaji wenye tajriba pevu katika maswala ya sheria waliozima mchakato wa BBI? Hatua hii ya Rais itazua malumbano makubwa wa kisheria nchini, watetezi wa katiba hii wakiwemo wanaharakati na wakenya kwa jumla watajitolea kupambana na Rais na serikali yake Kwa jumla kuhakikisha inatawala Kwa kuzingatia katiba.

Teuzi zote zifanywe kwa kuifuata katiba bila ubaguzi wala upendeleo. Rais ajue japo alifaulu kumaliza upinzani wa Raila odinga na viongozi wa upinzani nchini Kwa kuanzisha serikali ya handisheki kiasi cha upinzani kunyamaza hata serikali inapodhulumu wakenya, lakini aelewe wapo wakenya waliojitolea kupambana Kwa ajili ya kupatikana Kwa uongozi bora unaoheshimu katiba. Maadui wa katiba hawafai kupewa nafasi maana wanataka kurudisha nchi yetu katika mfumo wa kidikiteta tuliotupa kapuni baada ya kupita Kwa katiba mpya ya 2010. Jaji mkuu mpya Martha koome naye Msimamo wake juu ya swala hili la kudhulumiwa Kwa majaji wengine ndio utaamua ikiwa atafaulu kutetea haki na uhuru wa mahakama au wakenya watabakia kusadikishwa kulikuwa na mkono fiche wa serikali katika uteuzi wake. Enzi ya Maraga mkondo wa kuzingatia katiba ulikuwa umeshika kasi na Martha koome hatakuwa na lingine ikiwa lengo lake kweli ni kufuta mkondo wa maonevu na ukaidi wa katiba bila kujali tabaka, rangi, dini Wala mamlaka ya mtu.

Rekodi ya Rais uhuru imethibitisha anayo nia mbovu na mahakama kiasi cha kushindwa kuficha uhasama wake na idara hiyo . Wakenya wanajiuliza Kwa nini hasira ya serikali kupoteza kesi muhimu kortini zimchochee kiongozi wa taifa kugeukia majaji ambao si wanasiasa Bali lengo lao ni kutetea katiba tu kwa kuhakikisha inafuatwa na serikali au wananchi?.

Wakenya waliojitolea kupitisha katiba na ambao ushuru wao watumika kudumisha tume ya JSC na idara ya mahakama wanafaa kufahamishwa habari ambazo zilisababisha majaji hao kutemwa Katika orodha ya JSC.ni haki yao kujua kupata habari muhimu kutoka ikulu au Kwa idara ya ujasusi na za kuaminika juu ya swala hilo Kama inavyofafanunuliwa katika katiba yetu sura ya utangulizi, Rais hana hiari ila kukubali serikali yake iwe yenye kuzingatia misingi bora ya haki na usawa Kwa wakenya wote na utawala wa kisheria.

  • Tags

You can share this post!

Habari ndio hiyo!

Binadamu ndio wabaya!