• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Tujipange la sivyo tutapangwa, Kabogo ahimiza Mlima Kenya

Tujipange la sivyo tutapangwa, Kabogo ahimiza Mlima Kenya

Na LAWRENCE ONGARO

JAMII kutoka eneo pana la Mlima Kenya, imehimizwa kuja pamoja na kuzungumza kwa sauti moja.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu wakati mmoja, Bw William Kabogo, alishauri jamii hiyo isikubali kupangwa la sivyo “tutapangwa.”

“Sisi kama jamii ya Mlima Kenya tuna idadi ya watu wa kutosha ambao wakiamua kufuata mkondo mmoja wataleta mabadiliko makubwa. Kwa hivyo tusijitupe wenyewe,” alisema Bw Kabogo.

Aliyasema hayo kwenye hafla ya mazishi ya Bi Hellen Wanjiru, bintiye Bi Cecilia Wamaitha Mwangi aliyekuwa diwani wa Gatuanyaga hapo awali. Mazishi hayo yalifanyika katika boma la Bi Mwangi katika eneo la Gatuanyaga, Thika Mashariki.

Bw Kabogo alisema hakuna haja ya jamii ya Mlima Kenya kuacha chama cha Jubilee na kujiunga na chama kingine lakini akisema ni muhimu kufanya mazungumzo ya pamoja ili kupata mwelekeo wa kisiasa.

Hata hivyo, Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema “hata ingawa tunaendelea kuzungumzia maswala ya siasa, ni vyema kuzungumzia maendeleo kwani miradi iliyozinduliwa ni sharti ikamilike kabla ya kufika mwaka ujao wa 2022.”

“Hata hivyo, ninakubaliana na mwenzagu Bw Kabogo kwa ujumbe wake kwa jamii ya Mlima Kenya kuwa ni lazima tujiweke tayari kujadiliana na vyama vingine,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema huu sio wakati wa migawanyiko lakini ni vyema kuwa macho ili “jamii isipotoke.”

Naye mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina aliifariji familia ya Bi Mwangi akitoa ushauri wake kutoka katika Psalms 23 (4), ambapo maandiko yanasema kuwa: “Mungu ni mchungaji wangu ambapo nitapata chochote kwake iwapo nitanyenyekea. Ananiongoza kwa njia nzuri na kuniongeza nguvu maishani.”

Bw Patrick Wainana aliwataka viongozi kuwa na maono ya siku za baadaye.

“Kila viongozi ni sharti atimize ahadi yake kwa mwananchi kwani hiyo ndiyo sababu ya sisi kuchaguliwa na wananchi,” alifafanua mbunge huyo.

Alisema wakati wa uchaguzi ukifika kila mmoja atakuwa na jambo la kujitetea kwa mwananchi.

Viongozi walimsifu marehemu Wanjiru kama aliyejitolea mhanga kufanya kazi yake kwa bidii.

You can share this post!

Changamoto za kiufundi zachelewesha mpango wa kadi za...

Vigogo wapigania Karua kuunda muungano naye