• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Tuju apuuzilia mbali hatua ya Dkt Mutua kugura Azimio

Tuju apuuzilia mbali hatua ya Dkt Mutua kugura Azimio

NA CHARLES WASONGA

MKURUGENZI Mkuu wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya Raphael Tuju amepuuzilia mbali hatua ya Gavana wa Machakos Alfred Mutua kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza.

Akiongea na wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi Jumatatu, Mei 9, 2022, Bw Tuju alisema kuwa Dkt Mutua alikuwa anashinikiza apewe nakala ya mkataba wa Azimio ili aulinganishe na ule wa Kenya Kwanza.

Alisema kuwa viongozi wa Azimio walikuwa na habari kwamba Gavana huyo wa Machakos alikuwa ameanza majadiliano na mrengo huo unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

“Wengine wao walikuwa wakiongea na upande ule mwingine na walitaka stakabadhi hiyo kwa manufaa yao. Na kwa sababu tulikuwa tumepata habari za ujasusi kuhusu njama yao, hatukuona sababu ya kuendelea kuzungumza nao,” Bw Tuju akasema.

Dkt Mutua alisema kuwa aliondoka Azimio baada ya ombi lake la kutaka apewe nakala ya mkataba uliotiwa saini na vyama tanzu kugonga mwamba.

Hata hivyo, Bw Tuju alisema kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap hakuwa tayari kuunga mkono muungano wa Azimio bali alikuwa akitumia mkataba huo wa makubaliano kama kisingizio.

“Cheti cha ndoa huwa hakijengi ndoa. Kilichoko ndani ya stakabadhi hiyo sio muhimu, kile ambacho ni muhimu ni heri njema,” mkurugenzi huyo wa Azimio akasema.

“Wanajua kile ambacho walitia saini na waliisoma. Ikiwa ulitia saini bila kusoma, wewe ndiwe unafaa kujilaumu,” Bw Tuju akaongeza.

Dkt Ruto alitangaza hatua yake ya kugura Azimio kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi Jumatatu asubuhi.

“Tumeshawishika kwamba muungano ambao unaweza kuleta maendeleo nchini ni Kenya Kwanza chini ya uongozi wa William Ruto. Nina habari kwamba vyama vingine vitano vinapanga kugura Azimio kutokana an sababu na ulaghai na hatua ya kutenga maeneo fulani kwa vyama fulani,” Bw Mutua akasema.

  • Tags

You can share this post!

Alfred Mutua asema Kenya Kwanza nd’o mpango mzima

Mabingwa wa tenisi Afrika Mashariki U-14 Kenya warejea...

T L