• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Tunakamatwa kwa sababu mtoto mwenye maono amezaliwa jijini – Koech

Tunakamatwa kwa sababu mtoto mwenye maono amezaliwa jijini – Koech

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Belgut Bw Nelson Koech amedai kukamatwa kwake na wabunge wengine watatu Alhamisi katika eneo la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma ni njama ya kujaribu kuzima wandani wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto.

Mabw Koech, mbunge wa Kimilili Didmas Barasa, Wilson Logo (Chesumei) na seneta wa Nandi, Samson Cherargei walikamatwa kwa tuhuma za kuwa na silaha hatari kwenye magari yao, zinazodaiwa zingetumika kuzua ghasia na vurugu katika uchaguzi mdogo uliofanyika eneobunge la Kabuchai.

Uchaguzi huo ulizua ushindani mkali kati ya Joseph Majimbo Kalasinga wa chama cha Ford-Kenya, kinachoongozwa na seneta wa Bungoma Bw Moses Wetangula, na mgombea wa UDA, Evans Kakai.

Bw Kalasinga aliibuka kidedea kwa kuzoa kura 19, 274 akifuatwa na Kakai 6, 455.

Chama cha UDA kinahusishwa na Dkt Ruto, na kulingana na Bw Koech kukamatwa kwa wanasiasa hao wanne wa kundi la Tangatanga ni njama ya kuzima wandani wa Naibu wa Rais.

“Kuna mtoto aliyezaliwa jijini (akimaanisha chama cha UDA) na ‘serikali’ ina wasiwasi,” Bw Koech akasema.

Mbunge huyo alisema hayo Ijumaa, yeye pamoja na wabunge wenza waliotiwa nguvuni wakisubiri kufikishwa mahakamani kufunguliwa mashtaka.

“Lengo ni kuua motisha ya wandani wa Naibu wa Rais, tulishuhudia hayo wakati wa uchaguzi mdogo Msambweni,” Koech akadai, akilalamikia idara ya polisi na mahakama kutumiwa vibaya na serikali kuhujumu viongozi wanaoikosoa.

Wabunge hao wa Tangatanga walikesha katika kituo cha polisi cha Bungoma, Bw Koech akisema walikataa kuandikisha taarifa na pia kususia alama zao za vidole kuchukuliwa kwa kile alihoji “hatukuelezwa makosa tuliyofanya”.

  • Tags

You can share this post!

Nabulindo aahidi kuunganisha wakazi wa Matungu

Barasa: Waliozua fujo Kabuchai wangali huru, tunaonewa kama...