• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Tungali kwenye mataa baada ya kubomolewa makao

Tungali kwenye mataa baada ya kubomolewa makao

Na SAMMY WAWERU

NI zaidi ya miezi miwili tangu ubomoaji wa makazi na majengo utekelezwe eneo la Kware, Njiru, Kaunti ya Nairobi.

Ubomozi huo ulifanyika Machi 26, 2021 na kuendelezwa kwa muda wa siku kadhaa.Shughuli hiyo iliyoendeshwa chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya pamoja vya maafisa wa usalama, iliacha zaidi ya watu 5, 000 bila makao.

Jacinta Wanjiku Macharia ni miongoni mwa wahasiriwa wa ubomoaji huo, unaoutaja kuwa “haramu na uliokiuka haki za kibinadamu kipindi hiki taifa linang’atwa na virusi vya corona”.Wanjiku na ambaye ni mama wa mtoto mmoja, na chini ya wiki moja anasubiri kupata mtoto wa pili, anasema ubomozi ulianza alfajiri na mapema na hakuna alichoweza kunusuru.

Anaiambia Taifa Leo Dijitali kwamba mahandaki yalichimbwa ili kuzuia magari kuingia kubeba au kusafirisha wanachomiliki.“Tuliamshwa na gesi ya vitoa machozi iliyorushwa na maafisa wa polisi, hakuna tulichoweza kuokoa,” Wanjiku anasema.

Anaongeza: “Mahandaki yalichimbwa ili kutuzuia kuokoa tunachomiliki. Afisa mmoja wa polisi alinieleza amri imetoka juu,” anasimulia mama huyu.Makazi ya Wanjiku yalikuwa ya kwanza kuangushwa na matingatinga, yaliyosimamiwa na maafisa wa usalama.

Mama huyu anasema alitumia maelfu ya pesa kufikia alipokuwa, ila sasa amerejeshwa chekechea kuanza upya safari ya maisha.Hajui atakapoanzia ila ni mwingi wa matumaini Mungu atampa neema kustahimili mkumbo wa hasara na mazito yaliyomfika, na kuanza kupalilia maisha yake tena na ya familia yake.

Picha/ Sammy Waweru.
Jacinta Wanjiku Macharia anasema alilemewa na msongo wa mawazo baada ya nyumba yake kubomolewa, akionyesha dawa anazotumia.

“Ploti yangu niliinunua Sh330 mwaka wa 2018 na kuiboresha kwa zaidi ya Sh400, 000,” anafichua, akikadiria hasara ya ubomoaji huo.Kulingana na masimulizi yake, fedha hizo pamoja na mume wake walizikusanya kupitia kazi ya kijungu jiko.

“Mume wangu hufanya uchuuzi wa malimali kwa wilibaro, tulisaidiana kununua ploti na kuijenga huku nikifanya vibarua vya hapa na pale. Nikikumbuka tulivyojinyima kuondokea nyumba za kukodi Nairobi sina sababu yoyote ile ya kutabasamu kwa serikali,” anaelezea akionekana kuzongwa na mawazo.

Waathiriwa wakilalamikia kutendewa unyama na uhayawani, idara ya polisi nayo inasema ilikuwa oparesheni ya pamoja, na inapojiri haina majibu.“Ilikuwa oparesheni ya vikosi vya pamoja, na hilo linapojiri halina jawabu,” ansema Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kayole na ambacho kinajukumika kuimarisha shughuli za usalama eneo la Njiru, Bw Paul Wambugu.

Kwa mujibu wa viongozi wa serikali eneo hilo, ardhi hiyo yenye utata inamilikiwa na kampuni ya Njiru Ageria.Cheti cha umiliki wa ploti ya Wanjiku kinasema aliuziwa na mradi wa maskwota, unaomilikiwa na Investors Settlement Field, sawa na wanunuzi wengine.

Mama huyu akisubiri kujifungua juma lijalo, anasema hana mbele wala nyuma. Hajafanya maandalizi ya kutosha kukaribirisha malaika, mtoto wake wa pili.“Hata hivyo ninamshukuru Mungu kwa sababu ya tuzo ya uhai na kunijaalia mtoto wa pili, licha ya kuwa ninapitia mahangaiko chungu nzima,” Wanjiku anaelezea.

Baada ya makazi yake kubomolewa, Wanjiku anasema alilemewa na msongo wa mawazo ikizingatiwa kuwa yuko katika hali ya ujauzito.Alihamia katika mtaa wa mabanda wa Mukuru Kwa Reuben, kiungani mwa jiji la Nairobi.

Chumba chake, kimoja (single room) na cha mabati anachokodi Sh2, 000 kwa mwezi ki pembezoni mwa mto wa majitaka.“Mambo yalikuwa magumu na sikuwa na budi ila kutafuta huduma za matibabu,” akaambia Taifa Leo Dijitali wakati wa mahojiano nyumbani kwake, akionyesha dawa anazotumia kukabili msongo wa mawazo.

Isitoshe, mazingira anayoishi ni yale ya nyumba kusombwa na maji mvua ya mafuriko inapokunya.“Ninakoishi ni eneo ambalo huskia nyumba zinasombwa na maji wakati wa mafuriko na kuchomeka kupitia nguvu za umeme, siwezi nikaacha mwanangu humu ninapotoka,” Wanjiku akasema.

Licha ya hali yake, amelazimika kutumia stovu ya mafuta ya taa kufanya mapishi, jambo ambalo linahatarisha ujauzito wake.Akisubiri wakati wowote kujifungua kuanzia sasa, mumewe anaendeleza kazi yake ya uchuuzi.

“Kwa siku mauzo ya malimali yakiwa bora hakosi kupata Sh200, mapato tunayotegemea kukithi riziki na kusukuma gurudumu la maisha,” anadokeza.Huku serikali ikionekana kupuuza waliobomolewa makao yao Kware, Njiru, Wanjiku anasema amemuachia Mwenyezi Mungu yote aliyopitishwa.

Anaamini ipo siku atapata haki, hata ikiwa si hapa duniani, kwa waliotendea wahasiriwa wa Njiru unyama.“Tungali kwenye mataa baada ya kubomolewa makao, ila ninaamini Mungu yupo. Atatufungulia milango ya heri na Baraka,” Wanjiku anasisitiza.

Picha/ Sammy Waweru.
Jacinta Wanjiku Macharia akiwa kwenye chumba chake mtaa wa mabanda wa Mukuru Kwa Reuben, Nairobi akisimulia walivyofurushwa alfajiri na mapema Machi 26, 2021.
  • Tags

You can share this post!

Mtandao wa ‘Ardhi Sasa’ utaweza kuzima matapeli wa...

Sijapata hakikisho mastaa wa Kenya Simbas watashiriki mechi...