• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 10:18 AM
Tusisherehekee wabunge kupinga ushuru wa mkate

Tusisherehekee wabunge kupinga ushuru wa mkate

MAJUZI wabunge walikataa baadhi ya aina mpya za ushuru ambazo Waziri wa Fedha Ukur Yatani alipendekeza katika Mswada wa Fedha wa 2021 kwa lengo la kupata fedha za kufadhili bajeti ya kima cha Sh3.6 trilioni aliyosoma juzi.

Wamependekeza kuufanyia marekebisho mswada huo ili kuondoa ushuru mpya ambao waziri anapandekeza kutoza mkate, unga na pikipiki za uchukuzi maarufu wa bodaboda.Wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha walidai kuwa marekebisho hayo yanalenga kuwakinga wananchi wa kawaida wanaoathiriwa na janga la corona.

Kwa mtazamo wangu, ni mapema mno kwa Wakenya kusherehekea, hatua hiyo ya wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Homa Bay Gladys Wanga.Kwanza, hayo ni mapendekezo tu ambayo bado yanasubiri kujadiliwa katika kikao cha bunge lote lote kabla ya kupitishwa au kukatiliwa.

Pili, naona msukumo wa Bw Wanga na wenzake ni kuonekana kwamba wanawajali zaidi Wakenya wa kawaida kwa manufaa yao ya kisiasa ikizingatiwa kuwa zinasalia miezi 14 pekee kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao.

Kutokana na hali kwamba bunge la sasa limetekwa na kitengo cha Serikali Kuu, nahisi kwamba serikali itashinikiza kupitishwa kwa ushuru mpya zilizopendekezwa na Waziri Yatani.Hii ni kwa sababu imejitolea kuiwezesha Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kukusanya jumla ya Sh1.78 trilioni kufadhili bajeti hiyo ya mwaka wa kifedha wa 2021/2022.

Vilevile, mojawapo ya masharti ambayo Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) ni kwamba serikali iimarisha kiwango cha ukusanyaji ushuru kutoka nchini ili kupunguza mwenendo wake wa kuchukua mikopo kutoka nje.

Serikali ilikubali kutii sharti hilo na ndiposa shirika hilo lilikubali kuipa Kenya mkopo wa Sh255 bilioni za kuiwezesha Kenya kufadhili bajeti yake na kufufua uchumi wake ulioathiriwa na janga la Covid-19.IMF pia ilisema mkopo ambao iliipa Kenya itaisadia kupunguza mzigo wa madeni yake ambayo kufikia mwishoni mwa Mei ilikuwa imefikia kima cha Sh7.94 trilioni.

Isitoshe, katika bajeti ambayo Waziri Yatani aliyosoma bungeni mnamo Juni 10 mwaka huu, kuna pengo la Sh929 bilioni ambalo Hazina ya Kitaifa inatarajia kujaza kupitia vianzo vipya vya mapato (kama vile utozaji wa ushuru mpya) na mikopo kutoka humu nchini na nje.

Kwa hivyo, ushuru wa ziada ya thamani (VAT) wa asilimia 16, ambayo Waziri Yatani amependekeza utozwe mkate na unga ni miongoni mwa vianzo vipya vya mapato ambavyo serikali itategemea kufanikisha azma yake ya kufikia kiwango hitajika cha mapato.

Nakumbuka kwamba mnamo mwaka wa 2020, serikali ililazimisha kupitishwa kwa ushuru wa Sh18 zaidi kwa kila lita ya mafuta taa kwa kisingizio cha kupunguza visa vya kuchanganywa kwa bidhaa hiyo na dizeli au petrol.

Hii licha ya pingamizi kali kutoka kwa baadhi ya wabunge wa upinzani na wale wa mrengo wa chama cha Jubilee waliodaiwa hatua hiyo ingemuumizia raia wa kawaida ambao hutegemea mafuta taa kwa matumizi yao nyumbani.

Kile ambacho Rais Uhuru Kenyatta alifanya ni kurejesha Mswada wa Fedha wa 2020 bungeni na memoranda yenye mapendekezo yake ya kuitetea mswada pendekezo hiyo ya kuongezwa kwa ushuru huo wa mafuta.

Kisheria, memoranda kama hiyo ya Rais inaweza tu kubatilishwa na thuluthi mbili ya wabunge (angalau wabunge 233) idadi ambayo huwa vigumu kufikiwa.Bunge lilishindwa kufikisha idadi hiyo ya wabunge kuliwezesha kutupilia mbali mapendekezo yao Rais ya kudumishwa kwa ushuru huo wa Sh18 kwa bei ya mafuta taa.

Vivyo hivyo, licha ya wabunge kukataa ushuru zaidi kwa mkate, unga na pikipiki, Rais Kenyatta anaweza kutumia mbinu hii na kufanikisha utekelezaji wake. Hii ni kwa sababu hatua hiyo haitamwathiri kiasa kwa sababu anastaafu mwaka ujao.

  • Tags

You can share this post!

Hisia kali zazidi kuibuka kuhusu Kieleweke 5 kuhamia UDA

Ukosefu usalama huzorotesha uwekezaji katika nchi