• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Ukosefu usalama huzorotesha uwekezaji katika nchi

Ukosefu usalama huzorotesha uwekezaji katika nchi

Kwa muda sasa, wakazi wa jiji la Nairobi na viunga vyake wamelalamikia ukosefu wa usalama ambao umekua kutoka uchomozi, upokonyaji wa simu hadi wizi wa mabavu mchana.

Visa vya wakazi na wafanyabiashara kupigwa risasi na wezi vimeongezeka kila siku. Ujasiri wa wezi hao unatisha kwa sababu wanaonekana kutoogopa wanapotelekeleza uhalifu katikati mwa jiji kunakopaswa kuwa na usalama wa hali ya juu au kwenye mitaa iliyo na watu wengi.

\Wezi hao, wanaendelea kuwa wabunifu kila uchao unaowafanya kutekeleza uhalifu kwa urahisi, kusababisha maafa na kutoroka. Kulingana na wanaoshuhudia visa hivyo, baadhi ya wahalifu wanaonekana kuwa na ujuzi mkubwa wa kutumia silaha na kukwepa maafisa wa usalama ambao kila dalili zinaonyesha kwamba wanalemewa na jukumu lao la kulinda raia na mali yao.

Hii ni kwa sababu licha ya kukiri kwamba wanafahamu hali ya usalama imedorora jijini, hakuna hatua wanazochukua kukabiliana na hali hii kuwahakikishia raia usalama wao na mali yao. Alipozungumzia suala hilo wiki jana, Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai aliwataka waathiriwa kuripoti vituoni vya polisi taarifa hizi ili hatua zichukuliwe.

Kauli hii ni sawa na kuwakejeli Wakenya ambao wamechoka kutafuta msaada kwa polisi bila mafanikio. Wengi wamekuwa wakilalamika kuwa polisi hawachukui hatua Mkenya wa kawaida anapowasilisha ripoti kwao mbali wanachangamkia ripoti za mabwenyenye pekee ambao, wanavyodai, huwa wanawapatia pesa kushughulikia malalamishi yao.

Ripoti kadhaa zinasema ufisadi ni kama ibada kwa maafisa wa polisi.Madai haya ambayo yametoka sehemu zote za nchi hayawezi kukosa ukweli kamwe na yanaonyesha kuwa raia wa nchi hii wameachwa mikononi mwa wahalifu ambao hawaonekani kuwahurumia.

Ni kweli hali ngumu ya maisha inayowakabili raia wengi inaweza kuchangia wimbi la sasa la uhalifu jijini lakini hii haimaanishi kuwa polisi wanafaa kutelekeza jukumu lao la kulinda raia na mali yao. Uhalifu ukivuka mipaka, unadumaza, kulemaza na kuua uchumi wa nchi kwa kuwa hakuna mwekezaji anayeweza kuhatarisha maisha na mali yake akiwekeza.

Hivyo basi, hatua ya kwanza ambayo nchi hii inafaa kuchukua kufufua uchumi ni kuhakikisha kuna usalama wa kutosha sio tu katika jiji la Nairobi ambalo ni kitovu cha uchumi Afrika Mashariki, mbali katika nchi yote kwa jumla.

Hali inayoshuhudiwa kwa sasa ambapo watu wananyang’anywa mali mchana, kutekwa nyara na kupigwa ngeta inavyozidi, ndivyo matumaini ya kufufua uchumi yanavyodidimia. Huu ndio ukweli wa mambo ambao wanaoupuuza hujutia.

  • Tags

You can share this post!

Tusisherehekee wabunge kupinga ushuru wa mkate

Raia wakatae siasa chafu za uhasama