• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Ufisadi wavunja raia moyo wa kulipa ushuru – TI

Ufisadi wavunja raia moyo wa kulipa ushuru – TI

Na MARY WANGARI

KIWANGO cha juu cha ufisadi nchini kimewafanya Wakenya wengi kuwa na maoni mabaya kuhusu ulipaji ushuru, hatua inayolemaza utoaji wa huduma.

Kulingana na Shirika la Transparency International (TI), msimamo huo unatokana na kuwa wengi hawaoni thamani ya pesa wanazotozwa.

Mkurugenzi wa tawi la Kenya la TI, Bi Sheila Masinde, Alhamisi alitoa wito kwa serikali kuangazia kwa dharura vita dhidi ya ufisadi na suala kuhusu ukiukaji wa kanuni kuhusu ulipaji ushuru.

“Serikali inapaswa kuangazia suala kuhusu ukiukaji wa sheria kuhusu ulipaji ushuru ikiwemo ukwepaji ushuru na mengineyo ili kuwapa thamani walipa ushuru kwa pesa wanazokatwa.

“Kwa kawaida, viwango vya chini vya ufisadi huwapa motisha wananchi kulipa ushuru huku viwango vya juu vya ufisadi vikiwakatiza tamaa kuhusu kulipa ushuru,” alisema Bi Masinde.

Alisema haya katika warsha kuhusu maadili na kupiga vita ufisadi 2021, iliyohudhuriwa na Msimamizi Mkuu wa Bajeti Dkt Margaret Nyakan’go, Mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge dhidi ya Ufisadi Afrika (APNAC) Shakeel Shabir, afisi ya Mkaguzi Mkuu Matumizi ya Fedha za Serikali, miongoni mwa wengine.

Dkt Nyakan’go alisisitiza haja ya kuwapa wabunge mafunzo kuhusu usimamizi wa masuala ya umma, pamoja na ushirikiano kutoka kwa wadau husika ili kuboresha utendakazi wa idara hiyo katika kukabiliana na ufisadi.

“Afisi kama yangu haiwezi ikafanya kazi bila maafisa walio na utaalamu. Kwa utaalamu ninamaanisha ufahamu wa kanuni muhimu na uadilifu. Ni sharti tupunguze njia za mkato na tutie juhudi zaidi kuwaelimisha wabunge wetu kuhusu usimamizi wa fedha,” alisema.

Kwa upande wake, Bw Shabir alitoa wito kwa serikali kubadilisha mfumo wa ukusanyaji ushuru nchini kuwa wa wazi, ili kuhakikisha uwajibikaji na kuvutia imani miongoni mwa Wakenya.

Alifafanua kuwa mfumo wazi utawezesha raia kuona kiasi cha pesa wanachotoa na jinsi pesa hizo zinavyotumiwa.

“Shughuli ya ukusanyaji ushuru inapaswa kuwa rahisi na ya wazi, na ni sharti walipa ushuru waone thamani ya kutoa ushuru.

“Mfumo wa ukusanyaji ushuru haufai kuwa siri. Wananchi wanapaswa kujua ni kiasi kipi cha pesa wanachotoa, na ni jinsi gani fedha hizo zinavyotumiwa kuwezesha huduma kama vile za NHIF, NSSF na kadhalika,” alisema Bw Shabir ambaye pia ni mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Matumizi ya Fedha za Umma.

Dkt Sammy Sammy Kimunguyi wa afisi ya mkaguzi mkuu wa fedha za umma, alifichua kuwa visa vya uchunguzi wa kina kuhusu ukiukaji wa sheria kuhusu ununuzi vimeongezeka mno katika miaka ya hivi majuzi.

“Masuala yaliyogunduliwa na afisi yetu katika kipindi cha miaka miwili au mitatu iliyopita yanahusu ununuzi. Masuala makuu ni kukosa ushahidi wa sababu ya ununuzi, ukosefu wa mpangilio na ukiukaji sheria kuhusu ununuzi wa moja kwa moja,” alisema Dkt Kimunguyi.

You can share this post!

DOMO KAYA: Kaacha ustaa umtawale

Wanasiasa wa Mlima Kenya walia ‘kunyanyaswa’ na rais