• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Ujanja wa magavana wenye kesi kuendelea kuhudumu

Ujanja wa magavana wenye kesi kuendelea kuhudumu

Na WAANDISHI WETU

MAGAVANA waliozuiwa kufika katika makao makuu ya kaunti na kuendelea kuongoza kutoka kwa afisi zao kutokana na kesi za ufisadi, wametumia mwanya uliopo kwenye sheria kuendelea na majukumu yao huku kesi zao zikiwa zingali kortini.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) iliwashtaki magavana sita kwa kushiriki ufisadi huku Mike Sonko (Nairobi) na aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinard Waititu wakitimuliwa kutoka kwa uongozi wa kaunti na madiwani wa magatuzi yao.

Manyapara hao wa kaunti wamefasiri uamuzi wa korti kwamba wasifike katika makao makuu kuwa hitaji tu la kuwazuia kutekeleza kazi zao kutoka kwa afisi hizo. Hata hivyo, wanne waliosalia wamekuwa wakiendeleza majukumu yao kutoka kwa afisi nyingine nje ya makao makuu ya kaunti zao.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji mara kwa mara amelazimika kutoa ufafanuzi kwamba afisi zilizorejelewa kortini, zinajumuisha hata majukumu yao ya ugavana wala si mahali ambako afisi walizokuwa wakizitumia zinapatikana.

Katika Kaunti ya Migori, Gavana Okoth Obado amekuwa akitekeleza majukumu yake kutoka kwa makao rasmi ya gavana, eneo la Rapogi, kilomita 30 kutoka mji wa Migori. Amebadilisha iliyokuwa afisi yake kushughulikia kazi nyingine za kaunti ila majukumu mengi huwa anayatekeleza kutoka makao rasmi ya gavana ambapo kuna afisi kadhaa hata kwa wafanyakazi wa kaunti.

Wageni mbalimbali wamekuwa wakifika katika makao hayo kumtembelea Bw Obado huku mkurugenzi wake wa mawasiliano Nicholas Anyuor, akisema kuwa bosi wake amekuwa akifuata sheria na kutii amri ya korti.

Katika Kaunti ya Garissa, Gavana Ali Korane pia amekuwa akitumia makao rasmi ya gavana wala haendi katika zilizokuwa afisi zake tena. Bw Korane huandaa mikutano ya baraza lake la mawaziri pamoja na shughuli nyingine za kaunti katika makazi hayo ya kifahari.

Ingawa Bw Korane na Naibu wake Abdi Dagane wamekuwa na uhasama wa kisiasa kuhusu uongozi wa kaunti baada ya uamuzi wa korti, wazee waliingilia kati ili kuhakikisha kuna umoja na huduma kwa raia hazitatizwi.

Hali ni hiyo hiyo katika Kaunti ya Samburu ambapo Gavana Moses Lenolkulal amekuwa akiendelea na kazi zake kama zamani, akizindua miradi mingi ya maendeleo.

Kisheria, korti ilitarajia kuwa Naibu Gavana Julius Leseeto angekuwa akijihusisha na shughuli nyingi za kikazi zinazoandamana na afisi ya gavana baada ya Bw Leonolkula kuzuia kufika katika afisi zake.

Kati ya majukumu aliyoyatekeleza Gavana huyo ni kuteua kamati ya kupambana na janga la corona na pia mwaka jana alizindua ujenzi wa hospitali katika eneo la Archer Post.

Licha ya kusherehekea hadharani Gavana wa Tharaka-Nithi Muthomi Njuki alipozuiwa kufika katika afisi zake kutokana na kesi ya ufisadi, Naibu Gavana Francis Kagwima amesalia mtazamaji tu na hata kutengwa zaidi katika usimamizi wa masuala ya kaunti.

Bw Kagwima alikuwa ametangaza kuwa sasa ndiye kiongozi wa kaunti lakini Bw Njuki ameendelea kudhibiti masuala yote ya kaunti na hata kutoa amri ya utekelezaji wa sera mbalimbali.

You can share this post!

Balaa mikopo ya Kenya ikifika Sh9tr

Renato Sanches sasa andazi moto linalowaniwa Arsenal na...