• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Wakazi wa Thika kunufaika pakubwa ukarabati wa barabara ya kilomita 20 ukiendelea

Wakazi wa Thika kunufaika pakubwa ukarabati wa barabara ya kilomita 20 ukiendelea

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika na vitongoji vyake, watanufaika na ukarabati wa barabara ya kilomita 20 chini ya mpango uliofadhiliwa na serikali ya Kaunti ya Kiambu.

Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro, alieleza kuwa mradi huo wa barabara unastahili kukamilika chini ya miezi mitatu ijayo.

“Tunataka kuhakikisha vijana wetu wasio na ajira wanapewa nafasi ya kwanza wakati mradi huo unapoendelea,” alifafanua gavana huyo.

Kulingana na mipango yake vijana wapatao 90 wataajiriwa kazi ili kujihusisha na ukarabati wa barabara hiyo.

Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Alieleza kuwa vijana 30 watatoka mjini Thika, wengine 30 watatolewa katika kijiji cha Kiandutu, halafu idadi nyingine ya vijana 30 watatoka katika kijiji cha Ngoingwa.

Alieleza kuwa mpango huo utaleta mabadiliko makubwa katika eneo lote la Thika kwa sababu vijana wengi watapata ajira.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa wiki jana wakati wa uzinduzi wa barabara hiyo katika eneo la Ngoingwa, mjini Thika.

Alieleza wakazi hao kuwa kwa muda wa miezi tisa iliyosalia kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu mwakani, Kaunti ya Kiambu itafanya juhudi kuona ya kwamba miradi yote iliyozinduliwa wakati wa uongozi wake inakamilika mara moja.

“Tunajua itakapofika wakati wa kampeni viongozi wengi watakuja kwenu na lugha tamu wakiwaomba kura. Kwa hivyo ninawashauri muwe chonjo na viongozi hao kwa kuwachunguza zaidi,” alifafanua gavana huyo.

Alisema watu wa Mlima Kenya watatafuta kiongozi ambaye atawahakikishia amani na wawe na mazingira mazuri ya kuendesha biashara zao.

“Hatutamkubali kiongozi yeyote anayetumia matusi kutafuta kura za Mlima Kenya. Ni sharti pia kila kiongozi aheshimu afisi ya rais bila kuongeza matusi,” alieleza.

Wakati huo pia Askofu wa Kanisa la The Calvary Church mjini Thika, Bw David Kariuki Ngari, aliwashauri wakazi wa Thika wamchague kiongozi kutoka eneo hilo badala ya kutoka maeneo mengine.

“Nyingi wakazi wa Thika mumekuwa mkiwachagua viongozi wa kutoka nje ya mji wa Thika na ni wazi viongozi hao hawana mwelekeo mwema na nyinyi,” alifafanua Askofu Ngari.

Alisema yeye kama mzaliwa wa kijiji cha Munyu na kulelewa Thika angetaka kuwatumikia wakazi wa Thika kama mbunge wao.

“Ninakuja kwa unyenyekevu mbele yenu na kuwajulisha ya kwamba ningetaka mnichague kama mbunge wenu wa kutoka hapa Thika,” alijitetea kwa wananchi.

Alisema wakazi wa Thika wanahitaji kufanyiwa mambo mengi ya kimsingi na yeye kama mchungaji ana jawabu kwa hayo yote.

You can share this post!

KPA yatikisa tena kwa kuilemea Don bosco TZ

Kocha auchemkia uongozi wa Ingwe Leopards kuhusu mishahara

T L