• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 10:18 AM
Kocha auchemkia uongozi wa Ingwe Leopards kuhusu mishahara

Kocha auchemkia uongozi wa Ingwe Leopards kuhusu mishahara

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa AFC Leopards Patrick Aussems jana alizama mtandaoni kulalamikia njaa huku akikashifu uongozi wa klabu hiyo kwa kutojali maslahi ya timu hiyo.

Aussems, raia wa Ubelgiji alilalamika kuwa wanasoka, wafanyakazi na wanachama wa benchi ya kiufundi ya Ingwe hawajalipwa mishahara kwa miezi kadhaa huku uongozi wa Ingwe chini ya Dan Shikanda ukionekana kutoshughulishwa na hali hiyo.

“Benchi ya kiufundi, wafanyakazi na wachezaji wanakabiliwa na changamoto kadhaa. Hakuna mshahara, marupurupu na changamoto nyingine za kila siku. Hali hiyo inafanya kundi hili kukosa kuwajibika. Utepetevu wa baadhi ya watu?

Ukosefu wa heshima kwa fani hii? Natumai changamoto hizi zitashughulikiwa haraka iwezekanavyo,” akaandika Aussems kwenye ukurasa wake wa twitter.Kwa kuwa Ligi Kuu haina mdhamini, Ingwe imekuwa ikitegemea tu ufadhili wa kampuni ya Kamari ya Betsafe.

Mnamo Juni mwaka huu, Ingwe na Betsafe ziliafikiana kuwa udhamini wa miaka mitatu ambao ulikuwa wa Sh45 milioni, upunguzwe, kampuni hiyo ikisema kuwa hali hiyo imechangiwa na athari ya virusi vya corona.

Kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita, Aussems aliondoka na kurejea kwao kabla ya mechi yao ya mwisho dhidi ya Kakamega Homeboyz siku chache tu baada ya kurefusha kandarasi yake.Kuliibuka madai kuwa alikuwa ameigura Ingwe baada ya kuchelewa kurudi na kukosa mechi yao ya kufungua msimu dhidi ya Tusker.

Hata hivyo, aliwakosoa walioeneza madai hayo na hatimaye akarejea nchini na kuendelea kuinoa timu hiyo.Msimu huu umekuwa mgumu kwa Ingwe ambayo ilitorokwa na wachezaji wao tegemeo huku pia wakisajili siku ya mwisho kabla ya kipindi cha uhamisho kufungwa, baada ya kuondolewa marufuku ya Fifa.

Mabingwa hao mara 13 wa Ligi Kuu wamekuwa na mwanzo mbaya wa msimu wakishinda tu mechi moja ambayo ilikuwa dhidi ya Tusker mwanzo wa msimu. Wamepoteza dhidi ya Gor Mahia, Bandari, Sofapaka, Ulinzi na kupata sare tasa dhidi ya KCB.

Mwenyekiti wa Ingwe Dan Shikanda hakupokea simu kuzungumzia suala hilo ingawa ni jambo la wazi kuwa wachezaji wa Leopards wameenda miezi kadhaa bila kulipwa mishahara yao.Kauli ya Aussems inajiri wakati ambapo Ligi Kuu nchini bado imesimamishwa baada ya Waziri wa Michezo Amina Mohamed kuvunja Shirikisho la Soka Nchini (FKF) inayoongozwa na Nick Mwendwa.

Badala yake, Amina aliteua kamati ambayo itaratibu jinsi ambavyo ligi itaendeshwa kwa muda usiozidi miezi sita, kabla ya uchaguzi mwingine wa FKF kuandaliwa. Tayari kamati hiyo inayoongozwa na Jaji Mstaafu Aaron Ringera imetangaza kuwa ligi kuu itarajelewa wikendi ijayo na Leopards inafaa iwe imeanza kuimarisha maandalizi yake.

Wakati huo huo imebainika kuwa kampuni ambayo ilikuwa ikiendesha Ligi Kuu (KPL) huenda ndiyo itasimamia msimu huu baada ya uongozi wa sasa wa FKF kuvunjwa.

You can share this post!

Wakazi wa Thika kunufaika pakubwa ukarabati wa barabara ya...

Hatimaye mwafaka wapatikana Sudan

T L