• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:50 AM
Raia wakatae siasa chafu za uhasama

Raia wakatae siasa chafu za uhasama

Na MHARIRI

TAHADHARI iliyotolewa na viongozi wa makanisa hivi majuzi kuhusu uwezekano wa ghasia kutokea baada ya uchaguzi ujao, inafaa kutiliwa maanani.

Migawanyiko ya kisiasa ilianza kushuhudiwa punde tu baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita ambao pia ulikuwa umesababisha mgawanyiko mkubwa baina ya Wakenya wa matabaka mbalimbali.

Matumaini kwamba maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga yangeleta afueni hayakudumu kwa muda mrefu.Badala yake, kumekuwa na migawanyiko zaidi ndani na nje ya serikali ambayo inasababisha hatari ya machafuko baada ya uchaguzi ujao.

Kufikia sasa, tayari kumeshuhudiwa ghasia wakati wa chaguzi ndogo zilizopita na inahofiwa hali hiyo ikiendelea hadi wakati wa uchaguzi 2022 kutakuwa na maafa kando na uharibifu mkubwa wa mali ya umma.

Ni sharti wananchi wajiheshimu wenyewe na wakome kufuata wanasiasa wasio na chochote cha maana kitakacholeta maendeleo kwa maisha ya raia isipokuwa kueneza siasa za uchochezi.Kwa upande mwingine, wanasiasa wanafaa waonyeshe ukomavu kwa kukumbatia siasa za kunadi sera zao kwa wananchi badala ya kutumia mbinu hizo za kugawanya watu ambazo zimepitwa na wakati.

Viongozi wanaochochea ghasia hizi hawapatikani miongoni mwa wapinzani wa serikali pekee, bali pia kuna wale walio ndani ya serikali ambao husukuma wananchi kujitosa katika machafuko.Wakati serikali inapoamua kuonyesha ubaguzi uchaguzini, lazima walalamishi watataka pia wao watumie nguvu kujitetea.

Huu ndio uchochezi ambao hutoka kwa upande wa serikali.Taifa hili limepiga hatua kubwa kidemokrasia lakini inasikitisha jinsi suala la uchochezi wa kisiasa bado halijatatuliwa katika miaka hiyo yote.

Dalili ambazo zinaashiria uwezekano wa ghasia baada ya uchaguzi ujao ni kama vile miito inayotolewa na baadhi ya viongozi kuahirisha uchaguzi ili kuwe na nafasi ya kurekebisha katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI).Suala hili la kutaka uchaguzi uahirishwe linaweza kulipuka, kwani wanaotaka katiba ifuatwe kikamilifu wataanza kuzozana na upande ule mwingine.

Kando na haya, siasa za kikabila zingali zinatuandama katika baadhi ya maeneo ya nchi na hilo bado ni donda sugu ambalo linahitaji kutibiwa kwa haraka.Mbinu mpya ya baadhi ya wanasiasa wanaotumia umaskini wa Wakenya kama chambo cha kuwanasa kisiasa pia inahofiwa kuwa hatari kwa utulivu wa nchi.

  • Tags

You can share this post!

Ukosefu usalama huzorotesha uwekezaji katika nchi

Lissu kuzindua kitabu chake leo Nairobi